Sunday 13 September 2015

SAMIA AIBOMOA NGOME YA CUF


NA ABDALLAH MWERI, KIBAHA

MGOMBEA Mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameibomoa ngome ya chama cha CUF, baada ya Katibu wa chama hicho, Kata ya Kilangalanga, Mohammed Mfaume kujiunga na CCM.

Katibu huyo alisema ameamua kujiunga na CCM baada ya kuchoshwa na ubabaishaji unaofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa CUF.

Samia jana alifanya mkutano wa kampeni katika jimbo la Kibaha Vijijini ambapo aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kumchagua mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, mbunge wa jimbo hilo, Hamoud Jumaa pamoja na diwani wa CCM.

Alisema mwanachama huyo wa CUF, amejiunga na Chama baada ya kuchoshwa na usanii wa viongozi wa chama chake.

Samia alisema ujio wa kigogo huyo wa CUF, inadhihirisha kuwa CCM ni chama bora ambacho kinatekeleza vyema ilani ya uchaguzi.

Kwa upande wake, kigogo huyo wa CUF, alisema kitendo cha Juma Duni Haji kujiunga na CHADEMA kimeonyesha viongozi hao walivyopoteza mwelekeo.

Alisema Duni amefanya usanii kwa kuchukua kadi bandia ya CHADEMA kutokana na uroho wa madaraka na kwamba, ni mbabaishaji na amemtaka kuacha usanii kuhadaa wanachama wa CUF.

Kigogo huyo alisema alikitumikia chama hicho kwa uadilifu lakini hatua ya vyama vine kuungana na kujiita UKAWA kimeidhalilisha CUF hivyo hana sababu ya kuendelea kubaki.

“CUF nimeitoa mbali sana, zaidi ya miaka 10 nimekuwa kiongozi ulizeni hapa Kibaha nilikuwa mtu wa aina gani,” alisema.

Alisema kuanzia sasa atakuwa mwanachama mtiifu wa CCM na amerejea kuongoza nguvu katika kampeni ya mbunge wa jimbo hilo ili aweze kushinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema atakuwa mpiga kampeni mkubwa katika Chama ili kuhakikisha rais, mbunge na madiwani wa CCM wanapata ushindi mkubwa.

Hata hivyo alisema CUF imepasuka na kwamba wanachama wengi wa chama hicho Kibaha wanataka kurejea CCM.

Katika hatua nyingine, Samia alisema serikali itajenga soko la kisasa na stendi kubwa  ambapo wakazi wa Kibaha Vijijini watapata fursa ya kujiajiri.

“Soko na Stand itatoa fursa kwa wanawake, vijana kujiajiri pia tutaandaa utaratibu mzuri wa kuwarasimisha vijana kumiliki bajaji na pikipiki,” alisema.

Alisema serikali itajenga majengo ya halmashauri ya Kibaha Vijijini kwa sababu tayari kiwanja kwa ajili ya ujenzi kimepatikana.

No comments:

Post a Comment