Sunday 13 September 2015
DK. MAGUFULI KUHAKIKISHA AMANI, UTULIVU HAVIYUMBI
NA SELINA WILSON, MUSOMA
MGOMBEA Urais wa CCM, John Magufuli akipata ridhaa ya Watanzania, atahakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu ili kuharakisha maendeleo.
Amesema hakuna sababu ya watu kupigana mapanga wakati wote ni Watanzania na kwamba kila mmoja alizaliwa bila kuwa na chama.
Dk. Magufuli akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mkendo mjini Musoma, alisema anataka maendeleo ya haraka, lakini kama hakuna amani haiwezekani kuleta maendeleo.
“ Najua kiu ya Watanzania ni mabadiliko bora na sio mabadiliko ya kuwagawa na kuvuruga amani. Nawakumbusha wananchi tuna jukumu kubwa la kulinda amani.
“Pakikosekana amani huwezo kujenga barabara, pakikosekana amani hata ukiwa na ghorofa huwezi kulala ndani utakimbilia kujificha porini,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema amekuwa akiwaeleleza ukweli Watanzania kwa kuwa hana tabia ya kusema uongo na hata mungu hapendi uongo na anajua mabadiliko yatakuja kwa watu kufanya kazi.
Alionya juu ya mabadiliko ya kuwagawa Watanzania, akisema kwamba wananchi wanapaswa kujifunza yaliyotokea Kisumu nchini Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Libya na Sudan Kusini.
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alisema serikali yake itajenga uwanja wa ndege Musoma katika eneo la Nyasurula katika eneo la Musoma Vijijini ili kurahisisha usafiri na kufuangua fursa za ajira.
Aliahidi pia serikali yake itajenga kivuko kipya cha kubeba abiria na mizigo katika Ziwa Victoria ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali yanayotumia ziwa hilo.
Akizungumzia umeme na maji, Dk. Magufuli alimsifia Mgombea ubunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo , kwamba alifanya kazi kubwa alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kupeleka umeme vijijini hivyo atatumia umeme kujenga miradi ya maji.
Dk. Magufuli alisema kila kwenye umeme, atahakikisha anautumia kujenga miundombinu ya kusukuma maji kwenda kwa wananchi.
Kuhusu wafanyabiashara, alisisitiza kujenga na kufufua viwanda nchi nzima ili kuongeza ajira ikiwemo kiwanda cha nguo cha Musoma.
Aliwahakikishia wananchi katika serikali yake hatawaonea wafanyabishara ndogondogo kulipa ushuru wa hovyo unaowarudisha nyuma kimaendeleo na badala yake wafanyabiashara wakubwa ndio ayakaowasimamia walipe kodi.
“Sitaki watu wa bodaboda wasumbuliwe na askari kwa kukamatwa kamatwa kama ilivyo kwa mama ntilie. Kama ni kubadilisha sheria tutabaidilisha na kuunda mpya itakayokuwa rafiki kwa wafanyabishara wadogo,”alisema.
Alisema suala la ajira ni jambo muhimu hivyo, alisistiza kuongeza ajira na kwamba akiwa waziri wa ujenzi aliweza kutoa ajira milioni 1.1 kupitia makandarasi kwenye kazi za ujenzi.
Dk. Magufuli aliwanadi wagombea ubunge wa majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Mara, akisisitiza kwamba waichague CCM ili awe na safu ya watu wa kufanya nao kazi.
Mwigulu
Akihutubia wananchi wa Musoma Mjini, Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCmM na mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba, aliwataka wananchi wasikubali kurubuniwa na wapinzani.
Alisema mgombea wao, Edward Lowassa, wiki hii alitoa kauli ya kibabe akisema Watanzania wapende - wasipende ataingia Ikulu.
Mwigulu alisema mtu hawezi kuingia ikulu kwa ubabe na badala yake ataingia kwa kupigiwa kura na wananchi na mpaka msasa hata kura zikipigwa kesho mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, ndiye atakuwa Rais.
“Namtaka huyu bwana asiwatangulize wananchi kuingia ikulu kwa ubabe na badala yake atangulie yeye. Watanzania ni waelewa hawawezi kupeleka genge la wala rushwa Ikulu,” alisema.
Aliwataka wananchi wasikubali kupotoshwa na kauli za Lowassa kwamba akiingia ikulu ataipeleka nchi mchakamachaka na kasi ya hali juu wakati yeye mwenyewe anakwenda kwa mwendo wa kinyonga.
“Kukaa kwenye kiti ni kwa mwendo wa kinyonga, kuzungumza kwake mwendo wa kinyonga, kusimama kwake ni mwendo wa kinyonga, kutembea kwake ni kwa mwendo wa kinyonga je atawezaje kuwapeleka Watanzani mchakamchaka kwenye maendeleo,”alisema.
Mwigulu alisema CCM inajinadi kwa sera zake makini na mgombea wake bora Dk. Magufuli hivyo Watanzania kamwe wasikubwali kuchagua ukawa kwa kuwa hawana ajenda yoyote ya maendeleo.
Akizungumza kuhusu Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, alisema kwa miaka 10 aliyokuwa serikalini hajaweza hata kuwezesha shule zipate madawati na badala yake alitekeleza mikakati ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma na kujibinafsishia mashamba ya wananchi.
Alisema naye ni sehemu ya genge la wala rushwa ambao wamekuwa wakitumia kauli za baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kupotosha wananchi na kwamba dawa yao ni kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi chini ya Rais Dk. Magufuli.
Warioba
Kwa upande wake Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti waTume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliwataka wakazi wa Musoma Mjini wamchague Rais muadilifu na mchapa kazi.
Alisema anasikitishwa na kauli za kusema CCM haijafanya kitu kwa zaidi ya miaka 50 ambazo zinatolewa na waliokuwa watendaji wakuu wa serikali inadhihirisha kwamba wakufanya kazi yao sawasawa.
Makongoro
Naye Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, alisema Dk. Magufuli ni mgombea aliyepita kwenye mchujo ndani ya CCM na ni mtu ambaye kiwango chake cha utendaji ni cha juu.
Aliwataka wana Musoma wasichague watu wenye uchu wa madaraka ambao wameshindwa kukubali ndani ya CCM amekimbilia ukawa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment