Wananchi akishangilia wakati wa mkutano wa kampeni uliofanywa na Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan leo katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi |
Yajipanga kwa vurugu
baada ya uchaguzi
Kigogo CHADEMA afichua,
aiasa serikali
NA ABDALLAH MWERI
WAKATI Watanzania
wakijiandaa kupiga kura kumchagua rais, wabunge na madiwani Oktoba 25, mwaka
huu, CHADEMA imeendelea na mikakati ya kuzusha vurugu na imebainika kimepeleka
msituni zaidi ya vijana 3,000 kupatiwa mafunzo maalumu kwa ajili ya kutekeleza
mpango huo.
Tayari CHADEMA
imehusishwa kwenye matukio kadhaa ya vurugu zikiwemo zilizotokea wilayani
Kyela, Tarime, Dar es Salaam na maeneo mengi ambako wafuasi wake walivamia
mikutano ya wagombea wa vyama vingine na kuzusha vurugu.
Katika vurugu hizo, mtu
mmoja amepoteza maisha wilayani Tarime, huku maeneo mengine wananchi
wakijeruhiwa vibaya, ambapo ni utekelezaji wa mikakati na maagizo yanayotolewa
na viongozi wa chama hicho na vile vinavyounda kundi la UKAWA.
Mbali na hilo, viongozi
wa vyama hivyo mara kadhaa wamekuwa wakitoa kauli zinazoashiria kuna njama
mbaya ambazo wamepanga kuzitekeleza baada ya uchaguzi, ikiwemo kudai wataibiwa
kura na ile ya kuwataka wananchi kutoondoka kwenye vituo vya kupigia kura ili
kulinda kura za wagombea wao, jambo ambalo ni kinyume.
Hata hivyo, aliyekuwa
Katibu wa Uhamasishaji na Uenezi wa Vijana wa CHADEMA, Grayson Nyakarungu, amefichua
kuwa vijana hao 3,000 wamepelekwa msituni na sasa wanaendelea na mafunzo
maalumu.
Kigogo huyo, ambaye
ameamua kukihama chama hicho kutokana na mchezo huo mchafu na wa hatari kwa taifa,
alifichua siri hiyo katika mkutano wa mgombea mwenza wa urais, Samia Suluhu Hassan,
uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mailimoja Kibaha, Pwani.
Pia, alimkabidhi Samia rundo
la kadi za CHADEMA kutoka kwa vijana wenzake walioamua kurejea CCM, baada ya kuchoshwa
na ubabaishaji wa viongozi wa chama hicho.
Alisema wamefikia uamuzi
wa kukabidhi kadi za CHADEMA na kurejea CCM kwa sababu hawamkubali mgombea wa
urais wa chama hicho, Edward Lowassa.
"Huwezi kunishawishi
nimpigie kura Lowassa wakati alipokuwa CCM tulikuwa mstari wa mbele kumtaja
kuwa ni fisadi, leo CHADEMA imempokea huu ni ubabaishaji wa viongozi,"
alisema Nyakarungu.
Pia, alisema kigogo wa
CHADEMA, John Mnyika, hamkubali Lowassa na alikuwa akimuunga mkono aliyekuwa
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa, kumkataa Waziri Mkuu huyo wa
zamani aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond.
Nyakarungu alisema
CHADEMA ina vijana 3,000 ambao wako mafichoni wakipewa mafunzo maalumu ya
kujiandaa kufanya vurugu endapo Lowassa, atashindwa katika uchaguzi mkuu.
Alisema alikuwa miongoni
mwa viongozi wa CHADEMA akishirikiana na Mnyika, kuwakusanya vijana kutoka
katika maeneo mbalimbali nchini
kujiandaa na mapambano baada ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 25,
mwaka huu.
"Nilikuwa msaidizi
wa Mnyika kupanga mikakati ya kuandaa jeshi la vijana, ambao kwa sasa wako
msituni, kwa leo naishia hapa, mengi nitazungumza baadaye, mtu yeyote
akijitokeza kujibu," alisema Nyakarungu.
Kigogo huyo alisema
CHADEMA imejipanga kufanya vurugu baada ya kuona CCM imejipanga kikamilifu
kushinda katika uchaguzi huo wa urais, ubunge na madiwani.
Nyakarungu alivitaka
vyombo vya dola kufuatilia mwenendo wa CHADEMA kwa sababu chama hicho
kimejiandaa kuhatarisha usalama wa Watanzania.
"Niko tayari kutoa
ushirikiano kuhusu jambo hili, nina uhakika na maneno yangu kwa sababu mimi
nilikuwa mmoja wa viongozi nilioshiriki kukusanya vijana na kuwapeleka msituni
kwa mafunzo," alionya Nyakarungu.
Kigogo huyo aliwataka
wamiliki wa vituo vya mafuta na bandari kavu, kutofanya kazi Oktoba 25, mwaka
huu, kwa kuwa vijana hao wamepewa amri ya kuvamia na kupora muda mfupi baada ya
muda wa kupigakura kumalizika.
Akizungumzia kurejea
kwake CCM, Nyakarungu, alisema nyuma yake kuna idadi kubwa ya vijana ambao
baadhi yao walikuwa mafichoni, lakini wamerejea nyumbani kuimarisha chama.
Nyakarungu alimuomba
mgombea mwenza na viongozi wa CCM kuwapokea na wako tayari kuhamasisha vijana
wa Kibaha na maeneo mbalimbali kumchagua Dk. John Magufuli katika uchaguzi mkuu
ujao.
Alisema vijana waliorejea
CCM wataanza kazi ya kumpigia debe mbunge aliyemaliza muda wake, Sylvester
Koka, kupata kura za kishindo sanjari na kuwachagua madiwani wa chama hicho.
Kwa upande wake, Samia
alisema kuwa watafanya kazi na vijana hao kwa kuwa CCM ni chama madhubuti
ambacho kimejipanga vyema katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
"Karibuni nyumbani
na ninawapongeza. CCM ni chama imara ambacho kinatekeleza vyema ilani ya
uchaguzi, nawaomba tushirikiane tupate ushindi wa kishindo kwa kumchagua Dk.
Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano," alisema Samia.
No comments:
Post a Comment