Sunday 4 September 2016

JPM AWAONYA WANAOTAKA KUVURUGA MUUNGANO


RAIS Dk. John Maggufuli amesema wananchi wanapaswa kutambua sasa wanapaswa kuweka mbele suala la maendeleo na kuacha nyuma tofauti za vyama, kidini na kikabila.
Pia, ameonya mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga Muungano, atachukuliwa hatua kali za kisheria na kuwa katika kipindi cha wake atahakikisha unadumu.
Mbali na hayo amesema katu hatawaangusha watu masikini kwa kuwa ndiyo waliomchagua, hivyo atakwenda na kutembea nao.
Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Kibanda Maiti mjini Zanzibar, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua katika uchaguzi mkuu ulipita.
“Maendeleo yatakuwa ya pamoja..nataka kuona maendeleo kwa Watanzania, Wanzanzibari, Wapemba, tuweke vyama, dini na makabila pembeni na tuitunze amani yetu,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Alisema anataka kuona nchi inasonga mbele huku watu wakitii sheria bila shuruti na kiu yao kubwa ikiwa kuleta maendeleo.
Rais Magufuli alisema kilicho mbele yake ni kuona anawafanyia kazi bure masikini kwa kuwa walimchagua bure, hivyo kwa dhati aliahidi kutowaangusha.
“Nilichaguliwa na masikini, nitakwenda na masikini, nitatembea na masikini…nasema kwa dhati kuwa sitawaangusha,” alisema Rais na kuwa wananchi wanapaswa kuangalia walipotoka, walipo na wanapokwenda.
Alirudia kauli yake kuwa uchaguzi mkuu na ule wa Zanzibar umemalizika na kuwa utakaofuata utafanyika mwaka 2020.
“Uchaguzi mwingine ni 2020, wazunguke, waimbe hakuna kitu hadi kipindi hicho,” alisema Rais Dj. Magufuli.
Alitoa wito kwa wananchi kuwaepuka baadhi ya viongozi ambao badala ya kuunga mkono jitihada za keleta maendeleo, wamekuwa mstari wa mbele kufarakanisha.
Kutokana na hilo, alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuwa mnyenyekevu, mpole, mkarimu na anayewapenda watu wote licha ya baadhi yao kumfanyia vibweka.
“Rais Dk. Shein ana moyo wa tofauti na wapo watu wachache wenye moyo wa aina hiyo. Anampa mtu mkono halafu huyo mtu anakukatalia kukupa wake …lakini anaendelea kutumia mkono wake kutia saini posho za safari za nje, matibabu na ruzuku,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Mtu anayekataa kukupa mkono wako nawe unapaswa kukataa kutia saini mambo yake.”
Rais Dk. Magufuli alisema Dk. Shein kafanya mambo mengi ya maana kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo wanapaswa kumuunga mkono katika kipindi chake kilichobaki ili kufanikisha maendeleo yaliyokusudiwa.
Rais Dk.Magufuli aliwaasa wanasiasa kuwa wavumilivu na kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa kuwa madaraka yanayopata yanatokana na uwezo wa Mungu.
“Vyeo vinaletwa na Mungu…hata ungezunguka namna gani kama Mungu kasema hapana ni hapana,” aliasa na kuwa viongozi wanapaswa kutumia madaraka yao huko wakimweka Mungu mbele katika kutenda haki.

No comments:

Post a Comment