Monday 5 September 2016

KIZIMBANI KWA MAUAJI YA DADA WA BILIONEA MSUYA


MFANYABIASHARA wa jijini Arusha, Revocatus  Muyela (40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa tuhuma za mauaji ya dada wa  mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, bilionea marehemu Erasto Msuya, Aneth Msuya.

Kufikishwa mahakamani kwa mfanyabiashara huyo, mwishoni mwa wiki, kunafanya idadi ya watuhumiwa waliopandishwa kizimbani kuhusiana na mauaji ya Aneth, yaliyotokea Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, kufikia wawili baada ya awali mke wa bilionea Msuya, Miriam Msuya naye kupandishwa mahakamani hapo.

Mfanyabiashara huyo alifikishwa mahakamani hapo na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Bankika na kusomewa shitaka la mauaji na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo.

Wakili Diana alidai  mshitakiwa huyo Mei 25, mwaka huu, eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, alimuua Aneth.

Baada ya kusomewa shitaka, mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwani husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wakili huyo alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 6, mwaka huu na mshitakiwa huyo alirudishwa rumande hadi tarehe hiyo.

Agosti 24, mwaka huu, mke wa bilionea Msuya, Miriam alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Magreth, akikabiliwa na shitaka la mauaji ya
wifi yake huyo.

Miriam (41), mfanyabiashara na mkazi wa Sakina kwa Idd, Arusha, alikamatwa jijini Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kusomewa shitaka hilo.

Mke wa bilionea huyo, aliposomewa shitaka hilo, hakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Miriam alipelekwa rumande hadi Septembaa 6, mwaka huu, kesi hiyo itakapoletwa kwa kutajwa.

Agosti 9, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kumtia mbaroni mke wa bilionea huyo, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Aneth.

Aneth, ambaye ni dada wa bilionea Erasto Msuya, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana, nyumbani kwake eneo la Kibada block 16, Kigamboni, ambako inaelezwa wauaji hao hawakuchukua
kitu chochote ndani ya nyumba yake.

Bilionea  Msuya, aliuawa kwa kufyatuliwa risasi  katika eneo la Mijohoroni,  kando ya barabara ya Arusha – Moshi, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, akiwa ameitika wito wa kwenda kununua madini ya Tanzanite, baada ya kupigiwa simu na vijana wawili  waliomtaka wakutane maeneo hayo.

Inadaiwa alipofika katika eneo hilo, akiwa na gari lake aina ya Range Rover, T 800 CKF na kuwakuta vijana hao wakimsubiri, baada ya kuteremka, alikwenda kumsalimia mmoja wa vijana hao, ambapo kabla hajamfikia, alitoa bunduki aina ya SMG, namba KJ 10520, aliyokuwa ameificha kwenye koti na kumfyatulia risasi mwilini

No comments:

Post a Comment