Sunday, 12 June 2016

TRL KUNUNUA TRENI MBILI ZA KISASA


KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL), inatarajia kununua treni mbili za kisasa ili kukabiliana na msongamano wa magari katika mkoa wa Dar es Salaam.

Treni hizo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,000 kila moja na zitahudumia maeneo ya Ubungo, Pugu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Kaimu Mkurugenzi wa Mtendaji wa TRL, Masanja Kadogosa, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu siku 90 za utendaji wa uongozi mpya wa kampuni hiyo.

Kadogosa alisema treni hizo zitakuwa tofauti na zile zinazotumika  sasa, kwani zitakuwa na vichwa viwili kila moja, hivyo zikifika sehemu husika, hakuna haja ya kuvifuta vichwa na kuvihamishia sehemu inakokwenda.

Alisema treni zitakazonunuliwa zitakuwa mpya, hivyo hawatarajii kununua zilizotumika.

Kwa mujibu wa Kodogosa, tayari wameshazungumza na Benki ya Rasilimali Watu (TIB), kwa ajili ya kuwakopesha kiasi cha fedha na wamekubali  kufanya hivyo,  ingawa hakutaka kuweka bayana kiasi watakachokopa na lini wanatarajia kuzinunua treni hizo.

“Tayari tumezungumza na TIB na wamekubali kutukopesha kwa ajili ya kununua treni hizo za kisasa na tumeshawasilisha suala hilo wizarani, lakini hadi sasa hatuna bodi, hivyo tunasubiri bodi nayo tuweze kuieleza suala hili,”alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TRL alisema treni hizo zitakuwa zinatumia mafuta kidogo na gharama ya uendeshaji nayo itakuwa ndogo.

Alisema treni hizo zimetengenezwa kwa ajili ya abiria, hivyo kwa upande wa Pugu, ambako ni umbali wa kilomita 24, itakuwa inahudumia watu wa uwanja wa ndege pamoja na wageni wanaokuja nchini.

Akizungumzia kuhusu treni za jiji la Dar es Salaam, ambazo zinaendelea kufanya kazi, Kadodosa alisema mapato yameongezeka kutoka wastani wa zaidi ya sh. milioni moja hadi kufikia sh. milioni 3.3 kwa siku.

Alisema  ongezeko hilo ni asilimia 120, kwa mwezi uliopita, ikilinganishwa na Mei, mwaka jana.

Pia, alisema mapato ya treni ya masafa marefu yameongezeka kutoka sh. milioni 80.8, Mei, mwaka jana hadi kufikia sh. milioni 155.40,
mwezi, sawa na ongezeko la asilimia 92.3.

Alisema mapato hayo yanakwenda sambamba na kupunguza matumizi ya mafuta ya dizeli kwa vichwa vya treni kutoka asilimia 56 hadi 49. Alisema lengo ni kufikia asilimia 30.

No comments:

Post a Comment