Sunday, 12 June 2016

MAJALIWA: ATAKAYEDONOA MICHANGO YA MADAWATI KUKIONA CHA MOTO

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema serikali itamchukua hatua kiongozi yeyote atakayedonoa fedha za michango ya madawati inayotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Pia, amewaagiza watendaji wote wa serikali, walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, maofisa elimu, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, kuhakikisha michango hiyo inayotolewa inawafikia walengwa.

Aidha, amezitaka wilaya zote nchini zianzishe mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba, upungufu wa madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao na kwamba, utendaji wa viongozi wa elimu na serikali katika ngazi mbalimbali, utapimwa kutokana na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana, wakati wa matembezi ya hisani ya kukusanya fedha za kununulia madawati, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50, tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Katika maadhimisho hayo yaliyoanzia BOT hadi viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Gavana wa BOT, Profesa Benno Ndulu alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya shilingi milioni 263, zilizochangwa na benki hiyo pamoja na watumishi wake, kama mchango wao kwa ajili ya ununuzi wa madawati.

Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa BOT kwa kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto hiyo, ambapo alitoa wito kwa taasisi zote katika sekta ya umma na binafsi pamoja na watu binafsi, kuchangia uboreshaji wa elimu nchini, kama sehemu ya 'Majukumu ya Taasisi kwa Jamii'.

Alisema elimu bora sio tu faida kwa taifa, bali pia kwa waajiri,kwani itaziwezesha taasisi za umma na binafsi kupata wafanyakazi, ambao wameiva na wenye weledi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji katika taasisi hizo.

“Nitoe wito pia kwa wanafunzi wote, ambao watafaidika na kuboreshwa kwa mazingira ya kusomea, ikiwemo kupewa madawati na mahitaji mengine, kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa faida yao na taifa kwa ujumla na kwa kufanya hivyo, wanafunzi watakuwa wanaenzi jitihada za serikali, taasisi za umma, taasisi binafsi na watu binafsi katika kuboresha elimu nchini,” alisema.

Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano imeazimia kupambana na changamoto za sekta ya elimu na kwamba, tangu Uhuru, serikali za awamu zote zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali katika kuboresha elimu kwa wananchi wake.

Waziri Mkuu alisema mchango wa BoT kwa maendeleo ya taifa katika kipindi cha nusu karne ya uhai wake, ni wa kuigwa na taasisi zingine kwa kuwa pamoja na kushughulika na majukumu yake, ikiwemo kuhakikisha utulivu wa bei, uimara na uthabiti wa sekta ya fedha, utengenezaji na usambazaji wa sarafu na noti na ushauri wa kiuchumi kwa serikali, imekuwa kinara katika maendeleo ya jamii na taifa.

Alisema juhudi za serikali kupambana na changamoto ya sekta ya elimu kwa kuanza utaratibu wa kutoa elimu bure, moja ya matokeo yake ni kwa baadhi ya shule kama Shule ya Msingi Majimatitu, iliyoko Mbagala, kusajili zaidi ya watoto 1,000, waliojiunga na darasa la kwanza.

"Nimeguswa sana na hatua iliyochukuliwa na BoT kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kusaidia kutatua tatizo la ukosefu wa madawati. Nikiwa mwalimu na kiongozi niliyewahi kusimamia sekta hiyo, nawaonya wasimamizi wa jambo hili, yeyote atakaedonoa fedha za michango, atakiona. Tutachukua hatua haraka sana,”alisema.

Alisema hadi Machi 30, mwaka huu, kulikuwa na upungufu wa madawati milioni tatu, katika shule zote hapa nchini, ambapo kwa upande wa shule za msingi, mahitaji yalikuwa madawati milioni 2.8 na kwa shule za sekondari yalihitajika madawati 200,000.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitumia fursa hiyo kuiomba BoT, kuupa upendeleo mkoa wake kwa kupewa madawati mengi zaidi kwa kuwa mahitaji yake ni makubwa, ambapo yanahitajika zaidi ya 66,000.

Aidha, alimuomba Gavana Ndulu kuchagua barabara moja iliyopo katikati ya jiji, ambayo itakuwa ikitunzwa na BoT kwa kufanyiwa usafi, kupandwa miti na huduma muhimu huku akisisitiza agizo la kupaka rangi majengo yote mjini.

Naye Gavana Ndulu alisema mbali na mchango huo, BoT imeendelea kudhamini wanafunzi bora wa masomo ya uchumi na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia mfuko wa udhamini wa kumbukumbu ya Gavana wa tatu wa benki hiyo, Giltram Rutihinda, ambapo wanafunzi bora 31, wamenufaika, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

No comments:

Post a Comment