Sunday, 12 June 2016

JPM AMKUNA MO, AAHIDI KUMWAGA AJIRA 100,000


KASI na jitihada za Rais Dk John Magufuli katika kuongeza ajira kwa Watanzania, hususan vijana, zimeanza kuungwa mkono baada ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL), kutangaza mchakato wa kuzalisha ajira mpya hadi kufikia 100,000.

Hatua hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za Dk. Magufuli na tayari bilionea huyo kijana Afrika, anayemiliki METL, Mohammed Dewji 'MO', ameahidi kuongeza ajira hizo ili kukabili tatizo lililopo kwa sasa licha ya kampuni hiyo kuongoza kwa kutoa ajira nyingi nchini, ikishika nafasi ya pili baada ya serikali.

Kwa sasa, Dewji anayemiliki mtandao wa kampuni zilizo chini ya MeTL, ameajiri Watanzania 28,000, kupitia kampuni zake zaidi ya 31.

Akizungumza na jarida maarufu la uchumi duniani, Forbes la Marekani, toleo la wiki hii, MO alisema ameguswa na uchapakazi wa Dk. Magufuli, hivyo anajiona ana jukumu la kufanya katika kuisaidia serikali ya awamu ya tano kutokana na dhamira ya dhati ya kuinua uchumi wa nchi iliyoonyeshwa.

Alisema anakusudia kuajiri Watanzania 100,000, ndani ya miaka minne, ili aweze kutimiza ndoto yake ya kurudisha kwa wananchi sehemu kubwa ya faida katika biashara zake.

Aidha, alisema uamuzi wake huo umelenga kuwakwamua vijana na Watanzania ili waweze kujitegemea na kupiga hatua kimaendeleo, hali itakayosaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

MO amesema hayo ikiwa ni takribani wiki moja tangu kampuni tanzu ya MeTL Group, ilipong’ara katika Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka 2015 na kutwaa tuzo tatu, katika hafla iliyofanyika hivi karibuni, Dar es Salaam.

Katika tuzo hizo zilizoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na kuhudhuriwa na Rais Magufuli, kampuni zilizo chini ya MeTL ni Star Oils (T) Ltd, inayohusika na bidhaa za petroli, East Coast Foods & Fats, inayozalisha bidhaa za mafuta na sabuni na kiwanda cha nguo cha 21st Century cha Morogoro.

“Ninakusudia kuongeza dola milioni 500 zaidi (sh.trilioni moja) katika biashara zangu ndani ya miaka minne ili niweze kuajiri zaidi ya watu 100,000, wengi wakiwa Watanzania,” alisema bilionea huyo mwenye umri wa miaka 41, ambaye yumo katika orodha ya mabilionea 24, wakubwa zaidi Afrika, lakini akiwa namba moja kwa upande wa vijana.

Alisema miongoni mwa maeneo yatakayozalisha ajira mpya ni pamoja na kiwanda kipya cha sukari anachokusudia kukianzisha, akisema si kwamba kitazalisha sukari pekee, bali pia uzalishaji wa nishati ya umeme.

Akizungumza wakati wa tuzo hizo, Rais Magufuli alisema serikali yake imejipanga kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, watakaoanzisha viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.

Pia, alimuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuhakikisha anatengeneza mazingira yatakayowapunguzia kodi kwa kiasi kikubwa wawekezaji wa ndani na kupandisha kodi zaidi kwa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Alisema Tanzania ni nchi yenye utajiri wa rasilimali, fursa ya masoko, nguvukazi na mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo kipaumbele kikubwa kitakuwa ni kuhakikisha wazalendo wanapata fursa ya kufungua viwanda kwa wingi na kutumia ipasavyo fursa hiyo.

“Mchango wetu Afrika kiuchumi duniani uko chini ya asilimia tano, sasa ili tuweze kufikia malengo ya kukua zaidi kiuchumi, Afrika hatuna budi kufanya mageuzi ya sekta ya viwanda,” alisisitiza.

Rais Magufuli alisema endapo wafanyabiashara wa Tanzania watawekeza na kuanzisha viwanda nchini, watapata faida kubwa, wataiongezea nchi mapato, kuingiza zaidi fedha za nje na kutengeneza ajira kwa wingi.

Alisema kuendelea kutegemea na kutoa kipaumbele kwa bidhaa za nje hakuna faida zaidi ya hasara kwa Watanzania, kwa kuwa bidhaa hizo wakati mwingine huingizwa kwa njia za panya na kuwa bandia.

“Nimeshamwambia waziri wangu, serikali hii ya awamu ya tano inatoa fursa mtu kuwekeza popote hata kama ni mzalendo. Ukitaka kuwekeza kwenye mbolea, gesi, saruji, kilimo au mafuta, ruksa,” alisisitiza.

Rais Magufuli alisema lengo la serikali yake ni kuhakikisha sekta ya viwanda hadi kufikia mwaka 2020, iwe inachangia asilimia 40, kwenye pato la taifa na kuongeza uzalishaji wa ajira hadi kufikia asilimia 40.

MeTL Group, yenye utajiri wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja (sh. trilioni 2.2), ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 na imejikita katika sekta za biashara, kilimo, uzalishaji, nishati na petroli, huduma za fedha, huduma za simu, usafirishaji, usambazaji, majengo na miundombinu.

No comments:

Post a Comment