SERIKALI imeokoa sh. bilioni 25 kwa kuwaondoa watumishi hewa 12,246, kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa kipindi cha Machi Mosi hadi Mei 30, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora , Angellah Kairuki, alisema watumishi hao wameondolewa kwenye mfumo huo wa malipo ya mishahara kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni kutimiza umri wa kustaafu kwa lazima au kufukuzwa kazi, vifo, kuhitimishwa kwa mikataba na ugonjwa.
Angellah alisema fedha hizo zingepotea kama watumishi hao wasingeondolewa kwenye mfumo.
Alisema watumishi wengine hewa 10, 295 waliondolewa kwenye mfumo huo Aprili 3, mwaka huu, ambapo jumla ya sh. bilioni 23.2 ziliokolewa,
ikiwa ni ongezeko la watumishi 1,951, ambapo sh. billoni 1.8,ziliokolewa ndani ya mwezi mmoja.
Angellah aliwataka wakuu wa taasisi zote za umma na mamlaka za serikali za mitaa, kuwasilisha taarifa za watumishi hewa kabla ya
Juni 15, mwaka huu.
Alisema taarifa hizo zitasaidia kufanya tathmini na kupata uhakiki wa zoezi zima ili kuondoa watumishi hao na kuziwasilisha kwa Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumzia maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma mwaka huu, alisema yatadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi 23, mwaka huu na kauli mbiu ni 'Uongozi wa umma kwa ukuaji jumuishi kuelekea katika Afrika tunayoitaka'.
Aliwataka watendaji wakuu wa wizara, idara zinazojitegemea na wakala wa taasisi za serikali, kutenga siku moja kwa ajili ya kukutana na watumishi sehemu za kazi ili kusikiliza kero zao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment