Na Jonas Kamaleki-Maelezo, Dodoma
KAMBI rasmi ya upinzani bungeni, imemuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, katika juhudi zake za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo katika miradi ya maendeleo na huduma za jamii, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli.
Pongezi hizo zilitolewa juzi, mjini hapa na Mbunge wa Momba (CHADEMA), David Silinde, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2016/17.
“Tunamuunga mkono Rais Magufuli kwa kuondoa posho za vikao (sitting allowances) na tunamwomba aondoe posho hizo kwa wabunge nao watumie mishahara yao ili kuwe na usawa,” alisema Silinde.
Alisema kambi rasmi ya upinzani inaunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kukusanya kodi, ambayo inabidi ielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.
“Tunaiunga mkono serikali kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge, lakini tunamuomba Rais Magufuli apanue wigo wa kodi hiyo hadi kwa wakuu wa mikoa na wilaya,” alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Jimbo la Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema kambi hiyo inamuomba Rais Magufuli kufuta posho za vikao kwa wabunge ili kuleta usawa kwa Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment