ALIYEKUWA mfuasi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mwanachama wa CHADEMA, Goodluck Ole Medeye, amekihama chama hicho na kujiunga na UDP.
Mbali na kuhama, Ole Medeye amewapiga kijembe wabunge wa upinzani wanaounda UKAWA, wanaokimbia vikao vya bunge mjini Dodoma kwa kuwaambia kuwa, hizo ni siasa za kitoto.
Ole Medeye amesema madai ya kumkataa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ni hatua isiyoweza kubadili chochote, badala yake amewataka warudi bungeni.
Kuhama kwa Ole Medeye, kumehitimisha safari yake ya kisiasa iliyodumu miezi 11, tangu ahamie Chadema, Julai 29, mwaka jana, akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM), akimuunga mkono Lowassa, ambaye naye alihamia CHADEMA baada ya kukosa sifa ya kuwania urais kupitia CCM.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Arumeru Magharibi, alitangaza uamuzi huo jana, Dar es Salaam na kisha kukabidhiwa kadi ya uanachama na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi hiyo, Ole Medeye alisema amehamia kwenye chama hicho ili kufuata demokrasia ya kweli.
Ole Medeye amehamia UDP akiambatana na mkewe na watu wengine tisa, wakiwemo waliokuwa wanachama wa vyama tofauti na wengine waliodaiwa kutokuwa kwenye siasa, ambapo wote walijiunga na UPDP.
Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, alitaka kuunda chama kipya, lakini baada ya kupitia katiba za vyama hivyo, aliona UDP ni sehemu sahihi.
Alisema chama hicho kinasimamia haki na demokrasia hivyo anataka demokrasia ya kweli na jukwaa la haki ili kuwaletea Watanzania maendeleo ya haki.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wabunge wa kambi ya upinzani wanaosusia vikao bungeni, kurejea bungeni kwa sababu kususia vikao hakutabadili utaratibu wa kibunge, hususan kumuondoa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Wakati akiwa CHADEMA, Ole Medeye, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliteuliwa na vyama vya UKAWA kuwania nafasi ya Spika wa Bunge.
Katika kinyang’anyiro hicho, Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM), alishinda nafasi nafasi hiyo kwa kupata kura 254 dhidi ya 109 alizopata Ole Medeye.
No comments:
Post a Comment