Monday, 13 June 2016

MAJALIWA: TUUNGANE KUKOMESHA MAUAJI


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania na viongozi wa dini zote, kushirikiana kupiga vita matukio ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema anatarajia hali ya amani, usalama na utulivu itaendelea kuwepo nchini, hivyo wananchi hawana budi kushirikiana na kushikamana na serikali katika kuhakikisha maovu hayatokei katika maeneo yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi, mkoa Geita, alikokwenda kwa ajili ya kuhudhuria ibada ya kuwekwa wakfu, Padre Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.

“Mfano tukio la Mwanza, watu wanavaa kanzu na wanaingia msikitini na kukuta wenzao wanafanya ibada kisha wakawachinja. Hii haiwezekani kwa binadamu wa kawaida, hivyo tushirikiane katika kupiga vita matendo haya,” alisisitiza.

Majaliwa ametoa wote huo siku chache baada ya kutokea kwa mauaji ya kinyama, yaliyosababisha jumla ya watu 15, kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga katika mikoa ya Mwanza, Tanga, Dar es Salaam  na Mara.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga, amesema mkoani kwake kwa sasa, vitendo vya watu kuuawa kwa kukatwa mapanga vimepungua, baada ya kuanzisha kampeni maalumu ya kukemea mauaji hayo.

Alisema katika kampeni hiyo, wameamua kuwatumia walimu, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wauguzi, ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina, badala yake wajikite katika masuala ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili, zikiwemo za rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Amesema siku zote kumekuwa na ushirikiano mzuri kati ya serikali na asasi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madhehebu ya dini, katika kuwapatia wananchi huduma za kijamii kama vile, afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyinginezo.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa wito huo jana, wakati alipomuwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Mhashamu  Askofu Flavian Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.

“Serikali inatambua jitihada kubwa zilizowekwa na Kanisa Katoliki katika Jimbo hili la Geita na Tanzania kwa ujumla, hivyo wito wangu kwa Baba Askofu na waumini wa kanisa kwa ujumla wenu ni kuwaomba muendelee na kazi hii nzuri ya kutoa huduma muhimu kwa jamii,” alisema.

Amesema maendeleo ya nchi yanawategemea wote, hivyo ushirikiano  kati ya Kanisa na serikali utawezesha maendeleo ya Taifa kupatikana kwa kasi zaidi na kunufaisha wananchi wote.

Waziri Mkuu amesema jukumu la serikali ni kuweka mazingira wezeshi, ambayo yatasaidia Mtanzania kujikomboa na umaskini na kwamba, kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuunganisha jamii na wala siyo kuwatenganisha.

Waziri Mkuu amesema kinachotakiwa kufanywa na wote ni kumwuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kuwaelewa viongozi walioko madarakani na kutii maelekezo yanayotolewa kwani hata vitabu vya dini vinaelekeza kutii mamlaka.

Alisema iwapo waumini watatii na kuzingatia mafundisho ya kiroho yanayotolewa na viongozi wao wa dini, ni dhahiri kwamba yatajenga imani miongoni mwao na upendo utatawala katika jamii nzima.

Waziri Mkuu amesema serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, hivyo aliwasihi waendelee kuwekeza katika huduma za jamii, ikiwemo shule, vyuo na zahanati kwa kuwa wana jukumu la kushirikiana kwa pamoja kujenga taifa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwaomba wote kwa pamoja waunge mkono juhudi za Rais Dk. Magufuli katika kupambana na uzembe, ubadhirifu na wote wanaokiuka maadili ya utendaji wa kazi.

Kwa upande wake, Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo la Bunda, ambaye alikuwa msimamizi wa Kitume katika Jimbo Katoliki Geita, amewaomba waumini kumpa ushirikiano askofu mpya wa jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment