Monday, 13 June 2016
MCHUNGAJI MBARONI KWA KUMBAKA MWANAFUNZI
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kilokole la Victory Church, lililoko Sokoni One, mjini hapa, Chrisantus Mboya (35), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka muumini wake.
Mboya, anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa 17, mkazi wa Moshono, mjini hapa na kumsababishia maumivu makali.
Akithibitish kukamatwa kwa mchungaji huyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, alisema alitiwa mbaroni baada ya dada wa mwanafunzi huyo kutoa taarifa kituo cha polisi.
Alisema baada ya mchungaji huyo kuhojiwa na makachero wa polisi, ilibainika kuwa alimwita mwanafunzi huyo nyumbani kwake eneo la Sokoni One, jirani na kanisa hilo, saa 4;00 asubuhi, kwa kisingizio cha kumfanyia maombi.
Kamanda Ilembo alisema tukio hilo lilitokea Juni 6, mwaka huu na kuongeza kuwa, mtoto huyo alikuwa na matatizo ya kiafya.
Kwa mujibu wa Kamanda Ilembo, baada ya mchungaji huyo kumbaka mtoto huyo, alimtaka kuficha siri hiyo kwa kutomwambia mtu yeyote, kwa kuwa akifanya hivyo, atapata matatizo makubwa zaidi ya kiafya.
Hata hivyo, Kamanda Ilembo alisema baada ya mwanafunzi huyo kufika nyumbani kwa dada yake, Elizaberth Shadrack huku akiwa na maumivu, aliogopa kumjulisha kuhusu mkasa uliompata kwa mchungaji.
Alisema baadaye, dada wa binti huyo aliamua kuchukua simu ya mdogo wake na kukuta ujumbe wa maandishi kutoka kwa mchungaji, ukimuomba radhi kwa kilichotokea na kumtaka asimsimulie mto yeyote habari hizo.
Kamanda Ilembo alisema baada ya Elizabeth kukuta ujumbe huo, alimuhoji mdogo wake kuhusu kilichotokea nyumbani kwa mchungaji, ndipo alipomsimulia mkasa mzima.
"Ndipo dada mtu akaamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na mtuhumiwa alipopigiwa simu, alisema yupo eneo la Kimandolu, polisi wakamfuata huko na kumtia mbaroni,"alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa mwanafunzi huyo amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru, ambako anaendelea kupatiwa matibabu na kwamba, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wanaume wenye tabia hiyo, kuacha mara moja kwa vile ni kuwadhalilisha watoto wa kike. Alionya kuwa hatua kazi za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya vitendo hivyo.
Hivi karibuni, askari polisi wa Kikosi Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani hapa, Rafael Makongoro (25), alitiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya wasichana ya Korogwe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment