Tuesday, 14 June 2016
NASSARI, MADIWANI WANNE CHADEMA WATINGA KIZIMBANI
MBUNGE Jimbo la Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari na madiwani wanne wa chama hicho kutoka Halmashauri ya Meru mkoani Arusha, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kujibu shitaka la kuharibu mali kwa makusudi.
Mbali ya Nassari, madiwani waliopandishwa kizimbani jana, mbele Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Austino Rwizile ni Paulo Samwel, Japhet Jackson, Zefania Mwanuo na Anderson Sikawa.
Kabla ya kuwasomea shitaka hilo, Mwanasheria wa Serikali, Gaudensia Joseph alimuomba Hakimu Rwizile, kubadilisha hati ya mashitaka ya awali kwa ajili ya kumuunganisha Nassari pamoja na madiwani hao, katika kesi ambayo madiwani wenzao 24, walisomewa shitaka hilo katika mahakama hiyo Juni 8, mwaka huu.
Akisoma shitaka hilo, Gaudensia alidai kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Mei 4, mwaka huu, eneo la Leganga, Usa River wilayani humo.
Gaudensia aliendelea kudai kuwa, washitakiwa hao walivamia kiwanja kinachomilikiwa kihalali na mfanyabiashara, Itandumi Makere, kuvunja uzio na kuharibu mali zenye thamani ya shilingi milioni saba kwa makusudi huku wakijua kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, Nassari na madiwani hao walikana shitaka hilo, ambapo Wakili wa Utetezi, Charles Abraham akisaidiwa na Gift Joshua, waliiomba mahakama kuwapatia watuhumiwa hao dhamana kwa kuwa ni viongozi wenye anuani za kudumu na kesi yao ina dhamana kisheria.
Baada ya ombi hilo, Hakimu Rwizile alikubaliana nalo na kuwataka washitakiwa wajidhamini wenyewe kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini mmoja kwa kiasi hicho cha fedha.
Watuhumiwa wote walikidhi masharti hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu.
Idadi ya washitakiwa katika kesi hiyo imeongezeka na kufika 29 huku Nassari akiwa mshitakiwa wa kwanza. Washitakiwa wengine waliofikishwa mahakamani ni Nelson Wilium, Elisa Steven, Nelson Mafie,Wilson Fanuel, Digna John, Roman Laurence, Josephine Anael, Samwel Ismail, Agness Eliya, Izack Afitwa na Neema Izach.
Wengine ni Gadiel Stanley, Jeremia Masawe, Peter Efatha, Bernad Wilson, Hendry Benjamin, Emmanuel pendael, Fadhila Joseph, Penzila Palangyo, Merry Anton, Eveline Julius, Bryson Mosses na Frank Ngoye
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment