Tuesday, 14 June 2016

PROFESA LIPUMBA AOMBA KURUDI CUF

HATIMAYE aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, amerejea katika chama hicho na kuonyesha nia ya kutaka kurudi kwenye kiti hicho, alichokiacha miezi minane iliyopita, baada ya kukiacha wakati wa vuguvugu la uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana.

Profesa Lipumba amefikia uamuzi huo baada ya kuombwa na viongozi wa dini, wanachama na mashabiki wa CUF, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimbembeleza kurejea kwenye chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema tayari ameshamwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ya kutengua uamuzi wake.

Profesa Lipumba alisema tayari Maalim ameshaipokea barua hiyo, lakini kwa mujibu wa sheria, hajaijibu hadi utakapofanyika mkutano mkuu wa chama hicho, unaotarajiwa kuitishwa Agosti, mwaka huu.

Alisema alipojiweka kando na CUF, alitumia ibara ya 117 ya katiba ya chama hicho, inayoeleza namna viongozi wanavyoruhusiwa kujiuzulu katika wadhifa walionao na kwamba, hivi sasa anatumia ibara hiyo hiyo kurudi katika wadhifa wake.

“Barua yangu tayari ipo mikononi mwa Katibu Mkuu inashughulikiwa kisheria wakati nami nikiendelea na taratibu za kichama kusubiri majibu kutoka kwa mwanasheria wa chama,” alisema Profesa Lipumba.

Aliwaeleza wananchama wa CUF waliokuwa ukumbini hapo kuwa, hali ya kisiasa hivi sasa ni ngumu, hivyo  umoja kwa ajili ya kujenga siasa bora na demokrasia ya kweli ndani ya chama chao unahitajika kwa kiasi kikubwa.

Mbali na hilo, Profesa Lipumba aliunga mkono mafanikio yanayoletwa na Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli, hususan kwenye kupambana na rushwa, ukusanyaji kodi na kutoa elimu bure.

Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti Agosti 5, mwaka jana, kwa kile alichodai kutoridhishwa na hali ya mambo, ikiwemo umoja ndani ya UKAWA na kupokewa kwa aliyekuwa mgombea urais aliyeungwa mkono na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, Edward Lowassa.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na vuguvugu la wafuasi wa CUF kufanya makongamano nchi nzima, kutaka Profesa Lipumba arudi  kwenye madaraka  kwa madai kwamba, chama hicho kimekosa mtu imara upande wa Bara.

Wanachama hao wamekuwa wakishinikiza kuitishwa kwa mkutano mkuu maalumu kujadili hoja ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba kwa mujibu wa katiba ya CUF.

No comments:

Post a Comment