WAZIRI mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewaonya wananchi wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na kuwataka kuacha mara moja.
Badala yake amewataka wananchi hao watafute shughuli nyingine halali za kujiingizia kipato, vinginevyo wataishia pabaya.
Waziri Nchemba alitoa onyo hilo jana, baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, kuwa waziri wa wizara hiyo.
Mwigulu ameteuliwa kushika nafasi hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Charles Kitwanga, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na rais.
Kabla ya uteuzi huo, Mwigulu alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mbali na kutoa onyo kwa wafanyabiashara ya dawa za kulevya, Mwigulu alisema atahakikisha anasimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kuziba mianya inayohatarisha amani na utulivu nchini.
Kwa upande wake, Waziri mpya wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, amesema atahakikisha anashirikiana na wataalamu wa sekta tatu zilizo katika wizara yake ili kufanya mapinduzi katika maeneo hayo, yaliyoajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.
Waziri Tizeba pia alisema wizara yake itahakikisha inashugahulikia changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika, ambavyo vimekuwa havifanyi vizuri katika miaka ya hivi karibuni.
Mawaziri hao wawili waliapishwa jana na Rais Magufuli katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Dk. Tizeba ni mbunge wa Jimbo la Buchosa na alikuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.
Haya ni mabadiliko ya pili kufanywa na Rais Magufuli, tangu alipounda baraza lake la mawaziri, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Mabadiliko ya kwanza yalikuwa pale alipomuhamisha Profesa Makame Mbarawa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kwenda Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Mhandisi Gerson Lwenge.
No comments:
Post a Comment