Tuesday, 14 June 2016

KESI YA WABUNGE WANAODAIWA KUOMBA RUSHWA KUANZA JULAI 4



UPELELEZI wa kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 30, inayowakabili wabunge watatu, akiwemo wa Mwibala (CCM), Kangi Lugola, umekamilika hivyo imepangwa kwa kuanza usikilizwaji wa awali Julai 4, mwaka huu.

Mbali na Lugola, washitakiwa wengine katika kesi hiyo iliyoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa na wa Mvomero (CCM), Suleiman Sadiq.

Wakili  kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Godriver Kirian, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kwamba upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

Godriver alidai hayo wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa jana, ambapo aliiomba mahakama kuwapangia tarehe kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Simba alikubaliana na ombi hilo, hivyo aliahirisha shauri hilo hadi Julai 4, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali na kusema dhamana za washitakiwa zinaendelea.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, wabunge hao wanakabiliwa na shitaka la kujihusisha na vitendo vya rushwa, wakituhumiwa kuomba sh. milioni 30, kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, Machi 15, mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, iliyoko wilayani  Kinondoni, Dar es Salaam.

Inadaiwa washitakiwa hao wakiwa  wabunge na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya sh. milioni 30, kutoka kwa  Magotta.

Wabunge hao wanadaiwa  kuomba kiasi hicho cha fedha, kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment