Friday, 6 November 2015

KARIBU DK. MAGUFULI, KWAHERI RAIS KIKWETE


RAIS DK. John Magufuli ameapishwa kuwa Rais wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais na kuahidi atakuwa kiongozi wa Watanzania wote.

Ameahidi kuwa rais wa watu wote na kwamba serikali yake itakuwa na jukumu moja tu la kufanya kazi.

“Kwa ndugu zangu wa upinzani, nawaahidi kufanya kazi pamoja nao. Nyinyi mlikuwa washindani wangu katika kinyang’anyirio cha uchaguzi na si mahasimu.

“Uchaguzi umekwisha na Rais wa Tanzania ni John Joseph Pombe Magufuli, sasa hapa kazi tu,” alisema.

Akitoa shukran kwa maelfu ya watu waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana, Dk. Magufuli alisema anatambua imani ya Watanzania juu yake na kwamba kamwe hatawaangusha.

Rais Dk. Magufuli alisema katika serikali yake, atahakikisha anasimamia mambo yote kikamilifu na kwamba hatawaangusha.

Katika hotuba yake, Dk. Magufuli alimshukuru Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwa kuwa ndiye aliyemuibua na kumwamini kwa kumpa jukumu la kuwa waziri wa ujenzi katika kipindi chote cha uongozi wake.

Alisema hilo lilimtia moyo kwa kuwa wakati akiteuliwa kwa mara ya kwanza, akianzia kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, alikuwa na umri wa miaka 35 ambao ni mdogo mno.

“Namshukuru sana Mzee Mkapa kwa kuwa imani yake kwangu ilinijenga na kunitia moyo,” alisema.

Akimshukuru Rais Jakaya Kikwete, Dk. Magufuli alisema anatambua mchango wa Mzee Kikwete kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kushika wizara mbalimbali katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake.

Rais Dk. Magufuli alisema Rais mstaafu Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimpa fursa ya kuwa mgombea urais wa Chama katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

“Imani ya Mzee Kikwete ni kubwa mno. Namshukuru kwa kuniamini, naahidi kufanya kazi kikamilifu na kwa uadilifu ili kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo,” alisema.

Aidha, alimshukuru Rais mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, kwa kuwa busara zake zimesaidia kuiimarisha CCM na kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu.

Rais Magufuli alisema kazi ya Mzee Mwinyi ndani ya CCM katika kufanikisha uchaguzi huo ilikuwa kubwa na kwamba ndio chachu ya mafanikio yake na Chama kwa jumla.

“Wako wazee wetu wengi wastaafu wakiwemo mawaziri wakuu waliofanya kazi kubwa kwa kusimama imara na kuivusha CCM na nchi kwa jumla katika kipindi hiki kilichokuwa kikitazamwa kwa umakini zaidi,” alisema.

Katika salamu zake hizo za shukran, Dk. Magufuli alizipongeza taasisi mbalimbali zilizosimama imara kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu unafanyika kwa utulivu, haki na amani.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo ilisimama imara kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru.

Mbali na NEC, Dk. Magufuli pia alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vilifanyakazi usiku na mchana hadi kukamilika kwa uchaguzi huo.

“Nawashukuru waandishi wa habari kwa kuwa wamefanyakazi nzuri katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Tunatambua mchango wao,” alisema.

VIONGOZI WASHUHUDIA

Viongozi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake ni pamoja na marais Yoweri Museveni (Uganda), Robert Mugabe (Zimbabwe), Jacob Zuma (Afrika Kusini) na Joseph Kabila (DRC)

Wengine ni Paul Kagame (Rwanda), Phillipe Nyusi (Msumbiji), Uhuru Kenyatta (Kenya), Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn (Ethiopia), Makamu wa Rais Ponatshego Kedikilwe (Botswana), Makamu wa Rais Saulos Chilima (Malawi) na Waziri Mkuu  Barnabas Sibusiso Dlamini (Swaziland).

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Waziri Mkuu Saara Kuugongelwa (Namibia), Waziri Mkuu Jean Ravelonarivo (Madagascar) na Spika wa Bunge la Burundi.

Nchi zingine zilizotuma wawakilishi katika sherehe hizo ni pamoja na Algeria, Sudan Kusini, Oman, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na China.

Nchi zilizowakilishwa na mabalozi ni pamoja na Marekani, Ufaransa, Uingereza, Japan, Nigeria, Ghana, Sweden, Ushelisheli, Kuwait, Finland, Uholanzi, Denmark na Angola.

Mbali na nchi hizo, Jumuia mbalimbali za Kimataifa zilituma wawakilishi kwenye sherehe hizo ikiwa ni pamoja na Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), iliyowakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Richard Sezibera.

Kwa upande wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Stagomena Tax.

Kwenye sherehe hizo pia kulikuwa na wawakilishi kutoka Jumuia ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), Jumuia ya Madola, Umoja wa Ulaya (EU) na Mahakama ya Afrika.

Uapishwaji huo wa Dk. Magufuli pia ulishuhudiwa na watu mbalimbali maarufu akiwemo tajiri namba moja wa Afrika, Aliko Dangote na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga.

No comments:

Post a Comment