NA MOHAMMED ISSA
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju, amesema serikali imeokoa fedha nyingi za umma, baada ya kusinda kesi za madai.
Masaju alisema hayo jana muda mfupi baada ya Rais Dk. John Magufuli, kumwapisha kushika wadhifa huo, katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Aliwataka Watanzania kuendelea kufuata sheria zilizowekwa pamoja na kuilinda amani iliyopo.
Mwanasheria Mkuu huyo alisema ofisi yake inafanya kazi vizuri na kwamba imeiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi za umma, kutokana na kushinda kesi mbalimbali za madai.
Masaju alisema mwaka 2010, kulikuwa na kesi za uchaguzi 34, ambazo zote serikali ilishinda.
Aliwataka wananchi kufuata na kuzingatia sheria zilizopo ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.
Masaju alisema katika Bunge la 10, serikali ilijibu vizuri maswali yaliyoulizwa na kwamba katika Bunge la 11, atajibu maswali yote ya kisheria yatakayoulizwa.
Hafla ya kumwapisha Masaju ilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande; Spika wa Bunge, Anne Makinda; Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu.
Rais Dk. Magufuli amemwapisha Masaju ikiwa siku yake ya pili, tokea alipoanza kazi rasmi akiwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.
Kazi ya kwanza aliyoifanya baada ya kuapishwa juzi, ni kumteua Mwanasheria Mkuu na kuitisha Bunge.
No comments:
Post a Comment