Tuesday 5 January 2016

MAJALIWA APIGA MARUFUKU MAWAKALA KUNUNUA MAZAO




WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amepiga marufuku mawakala kutumika kununua mazao ya wakulima kwa niaba ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kutokana na mawakala hao kubainika kununua mazao ya wakulima kwa bei ya chini.
Imeelezwa kuwa mawakala hao wananunua mahindi kwa wakulima kwa bei ya sh. 180, kisha kuyauza NFRA kwa sh. 500, hivyo kusababisha wakulima kushindwa kunufaika na bei hiyo inayotumiwa na serikali kununua mazao hayo.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu ameiagiza NFRA kuweka vituo vya ununuzi wa mazao kwenye vijiji na kuhakikisha wanasambaza magunia ya kuhifadhia mahindi kwa wakulima ili waweze kuuza mazao yao kwa bei iliyopangwa na serikali.
Aidha, amesema serikali itaanda utaratibu maalumu wa kusambaza pembejeo za kilimo, badala ya kuwatumia mawakala, ambao wengi wao wamekuwa sio waaminifu na kusababisha malalamiko kutoka kwa wakulima.
Majaliwa alitoa agizo hilo juzi, wakati akikagua kituo cha kuhifadhia chakula mkoani hapa, ambapo alisema serikali haiwezi kuvumilia wakulima wakinyonywa na mawakala wenye kujali maslahi binafsi.
Alisema wakulima waendelee kulima mazao yao, hususan mahindi na serikali itayanunua kwa bei ya soko moja kwa moja pasipo kutumia mawakala.
“Haiwezekani mkulima alime mahindi kwa shida halafu wakala ayanunue kwa bei ya chini na kuyauza serikalini kwa sh. 500. Hii haivumiliki, hivyo NFRA kwenye msimu huu wa kilimo lazima mfungue vituo vya kununulia mahindi vijijini.
“Tunataka mkulima anufaike na bei iliyopangwa na serikali na sio mawakala, kama mawakala wanataka kunufaika na bei hiyo ya serikali nao watafute mashamba yao ya kulima,” alisisitiza.
Majaliwa alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa wanaotoa vibali kwa mawakala vya kununulia chakula kwa ajili ya kusambaza kwenye maeneo yaliyokumbwa na upungufu wa chakula, kuhakikisha chakula hicho kinafikishwa kwenye maeneo yaliyokusudiwa.
Aliongeza kuwa serikali itahakikisha hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kwa kukosa chakula kwa sababu chakula kipo cha kutosha.
Awali, kabla ya Waziri Mkuu kutoa maagizo hayo, mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama na mbunge wa jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Walemavu, walisema mawakala wamekuwa wakinufaika na bei ya mahindi iliyopangwa na serikali huku wakulima wakiendelea kunyonywa.
Wabunge hao walisema mfumo unaotumika na NFRA kununua mazao, hususan mahindi, haumnufaishi mkulima kwa sababu mawakala wamekuwa wakinunua mahindi kwa wakulima kwa wastani wa bei ya sh. 180 hadi sh. 200 kwa kilo.
Waliongeza kuwa licha ya wakulima kujitahidi kulima mahindi, bado hakuna soko la uhakika, hivyo waliiomba serikali kuweka utaratibu kwa wakulima wadogo kuuza mahindi kwenye hifadhi hiyo ya chakula.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa kauli hiyo, wakulima wa mkoa wa Ruvuma waliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Mkulima wa mahindi mkazi wa Peramiho, Ruth Michael, alisema maamuzi hayo yamewafanya kupata nguvu zaidi ya kulima mahindi kutokana na kupata uhakika wa soko la mazao yao.
“Waziri mkuu ametuongezea kasi ya kuendelea kulima mahindi kwa kuwa mawakala waliokuwa wakituvunja moyo kwa kununua mahindi kwa bei ya chini sasa mwisho wao umefika. Tutalima mahindi na kuyauza wenyewe kwa bei iliyopangwa na serikali na sio ya mawakala,” alibainisha.
Alisema walikuwa wakiuza mahindi kupitia kwa mawakala kwa bei ya chini kwa sababu walikuwa hawana sehemu nyingine ya kuuzia mazao yao.

No comments:

Post a Comment