Monday 28 August 2017

MUFTI ZUBERI ASEMA UISLAMU UNAVURUGWA


MUFTI wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi, ameonya kuwa dini ya Kiislamu nchini inavurugwa na baadhi ya watu, kiasi cha kufikia  hatua  ya kutojulikana kiongozi na anayeongozwa.

Amesema katika zama hizi, wajinga wamechukua nafasi huku wenye elimu sahihi ya dini ya wakinyamaza.

Kutokana na hali hiyo, amesema Waislamu wasio na ujuzi mkubwa katika masuala ya dini, wanashindwa kuelewa Uislamu sahihi unaostahili kufuatwa.

Mufti aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akifungua kongamano la siku mbili la  Walinganiaji, Maimamu na Wahutubu, kuhusu itikadi ya dini na mwelekeo sahihi wa dini ya Kiislaamu, lililoandaliwa na Taasisi ya People Committee of Charity ya Dar es Salaam.

Washiriki 60 walihudhuria kongamano hilo lililomalizika jana, katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

“Kila mtu anajisemea lake, anatoa fatwa (hukumu ya mambo ya dini). Kila mmoja sasa ni sheikh. Akisikia masheikh wakubwa wanaongea, anapinga anasema nani yule? Watu hawajui viongozi wana umuhimu gani?” Alihoji Mufti.

Aliongeza:" Kuna vijana wanaingia katika mambo mazito na magumu. Wanakwambia huo ndio Uislamu. Anakuwa na jazba, anataka kudhuru watu.
Utajiuliza Uislamu huu ameutoa wapi huyu, amejifunza wapi, kuangalia intaneti tu? Uislamu unapitikana kwa kujifunza miaka 30 hadi 40. Leo mtu siku mbili tu anajifanya anajua."

Alisema kwa sasa Uislamu unahitaji umoja kwa kuwa kuna changamoto nyingi na kubwa, zinazopaswa kutafutiwa ufumbuzi kwa pamoja.

“Uislamu ulianza kupata athari pale Waislamu walipoachana kila mmoja akawa na jambo lake.  Tulishughulika na kuminyana, kubughudhiana, tukaacha kusomesha vijana wetu elimu sahihi, maadili, kupenda nchi amani na elimu dunia,”alisema Mufti.

Alisema mpasuko katika Uislamu ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ukimya wa viongozi na wenye elimu ya dini hiyo.

“Kupitia kongamano hili, sasa mmeamua kuvunja ukimya na kuamua mseme, mfundishe na  tuzungumeze. Ni imani yangu kupitia hili, masheikh watatoa mwongozo wa dini sahihi ili maimamu na maustaadhi mkawaongoze wengine,”alisema.

Alisema makongamano, semina na hotuba zinaweza kuurudisha Uislamu ulio sahihi na maadili mema na hatimaye kuurejesha katika njia yake.

“Kuna matatizo makubwa katika jamii. Kikubwa nawaomba viongozi mwendelee kutoa elimu. Watu sasa hawajui nani wa kumfuata, yaani nyinyi masheikh au wale wanaoharibu sura nzuri ya Uislamu?” alisema Mufti Zuberi.

Aidha, alikumbusha kuwa Usilamu unahitaji amani katika utekelezaji wa ibada na nguzo zake, ikiwemo kutoa shahada, kuswali, kutoa zaka, kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kwenda kuhiji Makka.

Awali, Mratibu wa kongamano hilo, Sheikh Mbwana Ahmed Ulari, alisema madhumuni yake ni kuona umuhimu kwa ajili ya kuielewa itikadi sahihi ya Uislamu.

“Pia kuondokana na makundi yanayotangaza itikadi potofu katika jamii, yanayosababisha kuvurugika kwa amani na kumomonyoka kwa maadili na kuleta utengano,”alisema.

Alihimiza masheikh na maimamu kuandaa mada zinazofundisha uislamu sahihi ili waumini wasijiingize katika itikadi na utamadunini unaovuruga amani ya nchi.

No comments:

Post a Comment