Tuesday 29 August 2017

BOMOA BOMOA JANGWANI HAKUNA JIWE LITAKALOBAKI


SERIKALI imetangaza  kufanya operesheni kubwa ya kusafisha eneo la Bonde la Mto Msimbazi na kutoa ilani kwa wananchi wote waliovamia bonde hilo kuondoka mara moja kwa hiari.

Pia, imesema haitampa kiwanja wala fidia mtu yeyote anayeishi katika eneo hilo kwani wote ni wavamizi na wanaendesha shughuli zao isivyo halali.

Imesema operesheni bomoa bomoa awamu hii itakuwa ni kubwa na itahusisha vibanda na nyumba zote, ambazo ziliwekewa alama katika operesheni iliyofanyika mwaka juzi.

Mwanasheria wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manchare Heche, alisema nyumba 17,000, zinatarajiwa kuvunjwa katika operesheni hiyo.

Alisema operesheni itafanyika muda wowote kuanzia sasa na kuonya kuwa, hakuna mtu anayeishi ndani ya bonde hilo atakayesalimika.

“Kabla ya kufanya operesheni ya mwaka juzi, kulikuwa na nyumba 19,000 katika eneo hili. Tulivunja  nyumba 700 na zilibaki nyumba 17,000, ambazo nyingine ziliwekewa pingamizi mahakamani, lakini sasa hakuna kesi na tutavunja nyumba zote zilizosalia,”alisema mwanasheria huyo.

Alieleza kuwa eneo la Bonde la Mto Msimbazi ni hatarishi na serikali imelitenga kwa shughuli zingine.

“Pia, Bahari ya Hindi inapumulia katika bonde hili. Kwa miaka mingi watu wanakufa hapa kwa sababu  linakumbwa na mafuriko, vifo, mali zinaharaibika, hakuna mfumo mzuri wa kutiririsha mambo ya choo na huduma muhimu,”alibainisha Seche.

Alisema operesheni hiyo ya bomoa bomoa ilitakiwa kufanyika mwaka jana, lakini ilisitishwa ili wananchi waliokuwa wamesalia kuondoka kwa hiari.

“Ikumbukwe kuwa serikali inatumia fedha nyingi kufanya operesheni hizi. Tumeona wananchi wameanza kurejea tena hapa, hivyo ninatoa tahadhari waondoke kutii agizo hili la serikali kwa uzito wake,”alionya  Seche.

Ofisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Charles Mkalawa, alisema eneo la Bonde la Mto Msimbazi na Jangwani yote ni mali ya serikali siyo mtu binafsi, hivyo hairuhusiwi kufanya shughuli yoyote.

“Eneo hili lilipewa katazo la kuendeleza makazi au shughuli yoyote. Huu ni uvunjaji wa sheria, wanaokaa hapa wote ni wavamizi,”alisema Dk. Mkalawa.

Alisema wananchi waliovamia eneo hilo wasitegemee kupata viwanja vya bure wala fidia kwani serikali ilikwishatoa viwanja hivyo katika eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni kwa waliovunjiwa awali.

“Serikali iliwapa kwa huruma tu ya kibinadamu viwanja hivyo kwani walikuwa ni wavamizi. Huwezi kuvamia eneo halafu ukapewa na zawadi ya kiwanja. Awamu hii hakuna kiwanja kitakachotolewa,”alifafanua Dk. Mkalawa.

Serikali inatangaza kufanyika kwa operesheni hiyo, ikiwa ni siku chache tangu kuripotiwa sehemu ya eneo la Jangwani kudaiwa kupimwa viwanja na kuuzwa na wajanja wachache.

No comments:

Post a Comment