Tuesday, 29 August 2017

'LISSU ACHA KUITUMIA TLS VIBAYA'



RAIS wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, ametakiwa kuacha kukitumia chama hicho kuwa jukwaa la siasa na uanaharakati.

Pia, ametakiwa kuachana na mgomo, ambao unaweza kuharibu jitihada za serikali za kutaka mahakama ziendeshe kesi kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Smile Star Attorneys na Wakili wa kujitegemea, Leonard Manyama, alisema TLS isibadilishwe kuwa jukwaa la siasa, badala yake ibaki kushughulia masuala ya sheria.

Manyama aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuachana na mgomo uliotangazwa kufanyika leo na kesho.

Aidha, aliwataka wanasheria nchini kuendelea na kazi kama kawaida na wasubiri vyombo vya dola viendelee kufanyakazi yake.

"Serikali ya Tanzania ni yetu, hivyo tusijenge uadui ila tushirikiane ili tufike pale tunapopahitaji,"alisema Manyama.

Wakili Manyama alisema kufanya mgomo wa siku mbili ni kuwekeana chuki na wananchi, kitu ambacho siyo sawa kwa mujibu wa sheria.

"TLS haikuanzishwa ili kuwa chama cha siasa bali ni chama cha kutetea masuala ya sheria,"alisisitiza.

Wakili Manyama aliwataka Watanzania kulaani shambulio la mlipuko wa mabomu katika ofisi ya Kampuni ya Mawakili ya IMMMA, zilizoko barabara ya Umoja wa Mataifa, Dar es Salaam.

Naye, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma na Jeshi la Polisi nchini, wamekionya chama hicho kutoingilia vyombo vya uchunguzi na upelelezi vinavyochunguza tukio la mlipuko.

Profesa Juma alisema TLS haina haki ya kutoa agizo kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili ana mkataba binafsi na mteja wake.

Pia, alisema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanyakazi zake.

Alisema kwa kuwa tukio la kulipuliwa kwa ofisi za Mawakili wa IMMMA ni la kihalifu, wanasheria waache polisi iendelee na kazi yao.

"Kama kutatokea wateja watakaolalamika kuwa mawakili wao hawakufika mahakamani siku ya jumanne na jumatano, hatua za kisheria dhidi ya mawakili hao zitachukuliwa, ikiwemo kuwapeleka kwenye kamati ya maadili ya mawakili, "alisema Jaji Mkuu.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, limesema liachwe liendelee na kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo.

Msemaji wa jeshi hilo, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa, alisema jeshi hilo ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanya uchunguzi, hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa, anatakiwa kuzitoa polisi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Kauli hizo za polisi na ya Kaimu Jaji Mkuu, zimekuja baada ya Rais wa TLS, Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam, jana, kuwa, baraza lao la uongozi linazo taarifa kuwa, kikundi cha watu wenye silaha za moto, wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa Kampuni YA IMMMA na kuingia ndani ya eneo la ofisi hizo.

Lissu alidai watu hao baada ya kuingia ndani, walitega mlipuko na madumu manne ya mafuta ya petroli katika maeneo kadhaa ya jengo hilo.

"Kama Lissu anazo taarifa hizo, alitakiwa kulipoti polisi kwa kuwa ndicho chombo cha uchunguzi, siyo kuongea na vyombo vya habari,"alisema.  

No comments:

Post a Comment