Tuesday 29 August 2017

WANAODAIWA KUWATAPELI MAHUJAJI WANASWA


SIKU chache baada ya mahujaji kutoswa katika Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwashikilia viongozi wa taasisi zilizoratibu safari ya mahujaji hao kwenda Makka, Saudi Arabia.

Viongozi hao wanashikiliwa ili wahojiwe kutokana na tuhuma za kuwatapeli Waislamu 100, ambao walitakiwa kwenda kuhiji kupitia taasisi ya Twaiba na Hamarati.

Licha ya hatua hiyo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na polisi hivi karibuni wanatarajia kutoa tamko kuhusiana na suala hilo.

Chanzo cha habari hizi kimesema kuwa, mahujaji hao wanaweza kurudishiwa fedha zao au kukubali kusafiri mwakani, lakini itategemea na mwafaka na mazungumzo yatakavyoendelea.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, awali BAKWATA ilikuwa ikisimamia utaratibu mzima wa safari za mahujaji, lakini tangu taasisi zingine zilipoingila kati suala la kusafirisha mahujaji, kumekuwa kukiripotiwa malumbano mengi.

Hata hivyo, chanzo hicho kilisema  mwaka huu, BAKWATA ilifanikiwa kuratibu na kusafirisha mahujaji 113, kwa ajili ya kwenda kuhiji Makka.

Mahujaji wanaodaiwa kutapeliwa, walishindwa kusafiri baada ya kubadilishiwa ratiba ya safari yao.

Akizungumza jana, mmoja wa mahujaji hao, Seif Omar, alisema wamejitahidi kuwatafuta waratibu wa safari hiyo, lakini walishindwa kuwapata kwa kuwa simu zao zilikuwa zimefungwa.

"Tumetapeliwa kwani viongozi wa kampuni hizo walichukua tiketi zetu na visa na kudai wanazichukua kwa ajili ya maandalizi ya safari,"alisema.

Kwa upande wake, Yahya Ally, alisema taarifa walizonazo ni kwamba, viongozi wa kampuni zote mbili hawajulikani walipo.

Mahujaji hao walilazimika kwenda BAKWATA kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa safari yao, baada mambo kwenda kombo na kutakiwa wasubiri wakati baraza hilo likishughulikia suala hilo.

No comments:

Post a Comment