Tuesday, 29 August 2017

OPERESHENI MACHANGUDOA, MADANGURO YATIKISA TEMEKE


POLISI Mkoa Maalumu wa Temeke, katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewakamata  wasichana 34, kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao kingono, maarufu kama machangudoa.

Tayari Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Giles Muroto, ametangaza  operesheni hiyo kuwa ni endelevu na itahusisha pia msako wa madanguro, ambayo biashara ya ngono imeshamiri.

Usiku wa kuamkia jana, hali ilikuwa tete katika maeneo mbalimbali  wilayani humo, ambayo yanasifika kwa biashara ya ngono, kutokana na polisi kutapakaa kuwanasa wahusika.

Katika eneo la  baa maarufu ya Suger Ray, iliyoko Sokota na Mtoni Mtongani, polisi walifanikiwa kuwakamata wasichana 20, wakiwa ‘sokoni kujiuza’.

Operesheni hiyo pia ilitikisa katika eneo la Mbagala, ambapo wasichana 14, walikamatwa katika baa ya Masakuu, wakiuza miili yao.

“Usiku wa kuamkia jana, tulikamata  jumla ya wasichana 34, ambao tunawashikilia na tunaendelea kuwahoji. Ikibiainika wanajihusisha na biashara ya ngono, tutawafikisha mahakamani,”alisema Kamanda Muroto.

Alifafanua kuwa, kujiuza ni kosa  kisheria na pia biashara hiyo huchangia kueneza maradhi hatari na kuchochea uhalifu.

“Opresheni hii ni endelevu na hakuna dada poa atakayesalimika. Wafanye kazi halali,  siyo kuuza miili yao. Pia wanachochea uhalifu kwa sababu  wapo wanaoshirikiana na wahalifu,”alionya Kamanda Muroto.

Alieleza kuwa, operesheni hiyo inakwenda sambamba na kudhibiti madanguro, ambayo yapo katika makazi ya watu, hivyo kuwaomba wananchi wanaojua madanguro yalipo kutoa taarifa.

Katika hatua nyingine, Muroto alisema hali ya usalama kwa ujumla wilayani Temeke iko shwari, kutokana na polisi kuimarisha ulinzi na hakuna matukio makubwa ya uhalifu yaliyotokea.

No comments:

Post a Comment