Tuesday 29 August 2017

MANGULA AWAONYA WAGOMBEA WANAOTUMIA MAJINA YA VIGOGO


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukia wanachama wake wanaosaka uongozi kwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa Chama, ambapo kimesema watu hao hawauziki na hawana sifa za kuwa viongozi.

Kimewataka wapigakura kuhakikisha wanawanyima kura watu wote wanaokwenda kujinadi kwa kutumia majina ya viongozi wakuu wa kitaifa kwa kuwa wenyewe hawatoshi na hawawezi kusimama kwa miguu yao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, alisema hayo juzi, alipozungumza na Uhuru, kuhusu mtindo wa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali, kudai kuwa wametumwa na viongozi wa kitaifa kwa sababu wanahitajika kwenye Chama.

Mangula alisema viongozi wa Chama ndio wasimamizi wakuu wa Katiba, kanuni na miongozo, hivyo hakuna aliyemtuma mtu kugombea nafasi fulani ya uongozi kwa kuwa CCM inasimamia misingi ya haki na kutoa uhuru wa kidemokasia ili kila mwanachama mwenye sifa kugombea nafasi.

“Nimepata taarifa kwamba, watu wanakwenda mikoani kuomba nafasi za uongozi, wanasema wametumwana na viongozi, ama wao ndio chaguo la kiongozi fulani, jambo ambalo ni hatari kwa Chama.

"Sijamtuma mtu kugombea nafasi yoyote na hata Mwenyekiti wa CCM hajawahi kutuma mtu akagombee uongozi. Ukiona mtu anasema hivyo, ameshajitathmin ameona hauziki, ndio maana anatafuta jina la kiongozi mkubwa ili ajiongezee umaarufu ambao hana,”alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM, alisema Chama kimeweka utaratibu kwa mujibu wa kanuni na katiba yake, kila mwanachama anaweza kuwa kiongozi ili mradi akidhi vigezo, hivyo haiwezekani kutuma mtu akagombee nafasi fulani.

Aliwataka watendaji wa CCM katika ngazi mbalimbali, kuhakikisha wanasimamia kanuni na miongozo na kamwe wasimuogope mtu yeyote anayesema ametumwa kugombea na kiongozi kwa kuwa wao hawajatuma mtu.

“Tunafuatilia kwa karibu mwenendo wa wagombea wa nafasi mbalimbali, tukithibitisha mtu anasema katumwa na kiongozi ili kushawishi wapiga kura wamchague, tutamuondoa kwa kuwa hatoshi kuwa kiongozi kwa nafasi anayoomba,”alisema.

Mangula alisema viongozi wa CCM wa ngazi ya Taifa hawana safu binafsi za watu wanaotaka wawe viongozi , bali wamejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo ili kupata timu bora ya viongozi wa Chama, watakaokipatia ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama wa CCM, walisema mtindo huo wa kutumia majina ya viongozi umekuwa chanzo cha kupata viongozi wasio na sifa.

CCM inaendelea na uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kuanzia Septemba 20, mwaka huu, utafanyika katika ngazi za wilaya kwa jumuiya za Chama na baadae itakuwa ni zamu ya Chama ngazi hiyo kabla ya kuendelea katika ngazi za mikoa.

No comments:

Post a Comment