Monday, 28 August 2017

MAWAKILI WAITISHA MGOMO

CHAMA cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), kimewataka wanachama wake kususia kuhudhuria vikao katika mahakama, mabaraza mbalimbali kwa siku mbili kuanzia kesho hadi keshokutwa.

Maamuzi hayo yametangwazwa baada ya hivi karibuni, kutokea tukio la shambulio la mlipuko wa mabomu, katika ofisi ya Kampuni ya Mawakili ya IMMMA, zilizoko barabara ya Umoja wa Mataifa, Dar es Saalam.

Chama hicho kimesema, hatua hiyo ni sehemu ya ishara ya kuunga mkono na kupaza sauti ya pamoja na mawakili wa kampuni hiyo kwa kuonyesha kushutushwa na kulani tukio hilo.

Pia, kimesema kinatarajia kuandika barua kwa Jaji Mkuu, ili kumjulisha kutohudhuria kwa mawakili hao vikao vya mahakama siku ya Jummane na Jumatano.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Saalam, Rais wa TLS, Tundu Lissu, alisema hatua hiyo ni miongoni mwa maazimio ya Baraza la Uongozi wa TLS, yaliyotolewa kwenye kikao cha dharura, kilichofanyika Agosti 26, mwaka huu.

Lissu aliongeza kuwa, uongozi wa baraza hilo ulikutana na kujadili shambulio la mabomu dhidi ya ofisi za Kampuni ya IMMMA na ndipo ulipotoa maamuzi hayo.

"Baraza la uongozi linawataka wanachama wote wa TLS nchi nzima, kususia kuhudhuria katika mahakama na mabaraza ya aina zote kati ya Jumanne na Jumatano,"alisema.

Alisema chama hicho kina wajibu wa kuunga mkono na kulaani shambulio hilo, ambalo limewakuta mawakili hao, hivyo TLS inawataka mawakili wote nchini kutofanyakazi kwa siku hizo mbili.

Rais huyo wa TLS alisema anafahamu kufanya hivyo itatokea madhara makubwa kwa wateja wao, lakini kususia vikao hivyo ni kupeleka salamu kuwa chama hicho hakikubaliani na shambulio hilo.

No comments:

Post a Comment