Monday, 28 August 2017

UCHAGUZI WA CCM KATA 42 WAFUTWA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimefuta uchaguzi katika kata zake 42, kutokana na kuwepo kwa makundi ya uchaguzi uliopita na ukiukwaji wa Katiba na taratibu na Chama.

Kimesema, kata zilizofutiwa zinatakiwa kuandaa tena uchaguzi ili wanachama waweze kuchukua fomu za kugombea.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo za CCM zilizoko barabara ya Lumumba, Dar es Salaam.

Miongoni mwa kata zilizofutiwa uchuguzi na kutakiwa kurudia tena ni Kata ya Buguruni (mwenyekiti, katibu na katibu mwenezi), Kata ya Serya (UVCCM-katibu).

Nyingine ni Kata ya Liwiti (katibu) Kariakoo, Manzese, Pugu Stesheni (mwenyekiti, katibu na katibu mwenezi), Segerea (mwenyekiti na katibu) na Pugu (katibu mwenezi).

Alizitaja kata zilizofutiwa uchaguzi wote kuwa ni 18 za Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Liwiti, Makuburi, Mabibo, Kigamboni, Kiburugwa, Mchafukoge, Gerezani, Mianzini, Ndugumbi, Lilungule, Makumbusho, Kitunda, Ukonga na Msasani.

Nyingine ni Lumemo wilayani Kilombero mkoani Morogoro na Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo, Pwani.

Alisema kata hizo kuna baadhi ya watu, ambao bado wanaendeleza makundi ya uchaguzi mkuu uliopita na kupanga safu za uongozi.

"Tumefuatilia uchaguzi unavyoendelea, zipo changamoto, katika maeneo machache hayakwenda vizuri. Tumeona leo tutoe kauli kwani tusingependa kuona uchaguzi huu unanajisiwa na vitendo na mienendo ambayo inakwenda kinyume na mageuzi ya CCM," alisema.

Aliongeza: "Kuna maeneo mengine, viongozi wameshindwa kutoa usimamizi mzuri wa mali za Chama na kusababisha upotevu mkubwa, lakini bado wamerejea kwenye uongozi. Hili halikubaliki."

Pia, alisema mtu yeyote anapogombea uongozi CCM, lazima awe mkazi wa eneo husika, siyo vinginevyo. "Kama siyo mkazi wa eneo hilo, haupaswi kugombea katika eneo hilo," alisisitiza.

"Sasa wapo baadhi ya watu katika maeneo machache siyo wakazi wa maeneo hayo na wameomba dhamana katika maeneo, ambayo wao siyo wakazi. Hili halikubaliki," alisema.

Vilevile, alisema katika maeneo mengine, kumekuwepo na vitendo vya uonevu na kutokutenda haki kwa wanachama.

"Kuna maeneo mengine vikao havikupewa taarifa kuhusu wagombea. Hili halikubaliki kwa sababu unapotosha vikao," alisema.

Polepole alisema CCM imejipanga kupata viongozi, ambao ni waaminifu, waadilifu, wachapakazi, wenyenyekevu na ambao wanaweka mbele maslahi ya taifa na Chama.

"Ni viongozi wapole, lakini wakali sana kwa mambo yasiyofaa, ambao wapo tayari kuwatumikia Watanzania kwa moyo wao wote na nguvu zao zote. Hawa ndiyo aina ya viongozi ambao wanachama wa CCM wanatuletea," alisema.

Alisema uchaguzi huo unaofanyika mwaka huu, ni sehemu ya mageuzi makubwa, ambayo yana lengo la kukirejesha Chama kwa wanachama.

Alipoulizwa watawachukulia hatua gani viongozi waliohusika kuharibu uchaguzi huo, alisema: "Chama chetu kinaongozwa kwa mujibu wa katiba. Kama kuna kiongozi amekiuka kanuni ya maadili ya Chama, kamati yetu ya maadili itakaa na kuwahoji watu hawa na kuchukuliwa hatua stahiki."

Pia, alitoa rai kwa viongozi wa Chama kuendelea kusimamia katiba, kanuni ya uchaguzi na maadili katika kipindi hiki cha uchaguzi wa chama.

"Uongozi wa Chama chetu unamaanisha tunaposema, tunataka aina ya viongozi ambao ni waadilifu, waaminifu na wachapakazi," alisema.

No comments:

Post a Comment