Monday, 28 August 2017

HOSPITALI YA KAIRUKI YAINGIA MATATIZONI


NA FURAHA OMARY

MKAZI wa Dar es Salaam, Khairat Omary, ameifungulia kesi ya madai Hospitali ya Kairuki, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiiomba iamriwe kumlipa sh. milioni 155.

Khairat, amefungua shauri hilo la madai namba 184 la mwaka huu, kupitia Wakili wake, Jonas Nkya wa Jonas & Associates Law Chambers.

Katika hati ya madai, mlalamikaji huyo pamoja na mambo mengine, anaiomba mahakama kuamuru mlalamikiwa kumlipa kiasi hicho cha fedha, kutokana na matatizo ya afya aliyoyapata, yakiwemo ya kuondolewa kizazi  kutokana na hospitali hiyo kushindwa kutimiza wajibu wake.

Shauri hilo limepangwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo litatajwa Alhamisi ijayo.

Kupitia hati ya madai, Khairat anaiomba mahakama imwamuru mlalamikiwa kumlipa sh. milioni 20, zikiwa gharama za tiba na matibabu na gharama za dharura alizotumia, sh. milioni 25 kwa ajili ya kupoteza kipato, sh. milioni 80 gharama za adhabu, sh. milioni 30 za kuvunja wajibu wake.

Pia, anaiomba mahakama imuamuru mlalamikiwa kumlipa riba ya asilimia 21m tangu tarehe ya kuvunja wajibu wa huduma hadi tarehe, ambayo itatoa hukumu, baada ya kuridhika na madai hayo na gharama za kesi na amri nyingine  ambazo  itaona zinafaa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, inadaiwa mlalamikaji alikuwa mteja wa mlalamikiwa, akihudhuria  kliniki ya ujauzito kwenye hospitali hiyo, ambapo wakati huo hakuwahi kuwa na tatizo lolote na alipangiwa kujifungua kwa njia ya kawaida Desemba 15, mwaka jana au kabla ya tarehe hiyo.

Inadaiwa Desemba 15, mwaka jana, alipokewa hospitali hapo na kujifungua mtoto kwa njia ya upasuaji, ambapo siku mbili baadaye, Desemba 17, mwaka jana, aliruhusiwa  na kutakiwa  kurudi hospitalini hapo kwa ajili ya kuangalia afya yake Desemba 21, mwaka jana.

Inadaiwa baada ya kufika nyumbani, mlalamikaji alianza  kupata maumivu chini ya tumbo, kichefuchefu na kutapika, hivyo Desemba 21, mwaka jana, aliporudi  hospitalini hapo, alilalamika kwa daktari aliyemhudumia kuhusu maumivu makali na matatizo mengine, yakiwemo ya kutokwa na uchafu ukeni.

Mlalamikaji anadai daktari aliamuru akafanye kipimo cha (ultra sound) ili kufahamu tatizo, ambapo baada ya hapo, alipatiwa dawa za kutuliza maumivu na kuambiwa atajisikia vizuri.`

Hata hivyo, baada ya kufika nyumbani, hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi, ambapo alikuwa na homa kali, kichefuchefu, kutapika na tumbo lilianza kuvimba na kubadilika rangi, jambo lililomfanya ashindwe kutembea mara kwa mara.

Mlalamikaji anadai alienda hospitali ya karibu, ambapo ilibidi ahamishiwe Hospitali ya Regency, kwa matibabu zaidi, ambako baada ya kuona hali yake, ilibidi ahamishiwe  Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Inadaiwa baada ya uchunguzi, madaktari walishauri aondolewe kizazi kutokana na kuharibika kwa kuwa waliacha vitu vilivyotumika kwa ajili ya kumzalishia, ikiwemo pamba.

Anadai amepata matatizo ya fistula na  hana nafasi tena ya kuweza kupata mtoto huku ikizingatiwa ana umri wa miaka 29.

No comments:

Post a Comment