Tuesday, 3 January 2017

JPM AVUNJA KAMATI YA MAAFA KAGERA, AAGIZA MATUMIZI YA FEDHA ZOTE YAFUATILIWE

RAIS Dk. John Magufuli ameivunja rasmi kamati ya maafa iliyokuwa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, ili kutoa nafasi kwa kiongozi huyo kushughulikia masuala yanayohusu maendeleo ya wananchi.

Amesema mpaka sasa ni mwezi wa tano tangu kuundwa kwa kamati hiyo na kwamba, siyo ajabu wajumbe wanalipana posho, hivyo ni muda muafaka ikasimama na kila kiongozi kuendelea na masuala mengine.

Pia, ameiagiza Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kufuatilia matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya maafa ya tetemeko la ardhi
lililotokea, Septemba 10, mwaka jana, mkoani Kagera.

"Kwa sasa haya maafa yamekwisha, mkuu wa mkoa nenda kashughulikie wananchi wafanye kazi kwa sababu ili maendeleo yaje, ni lazima serikali ifanye kazi na watu wafanye kazi.

"Licha ya hilo, nataka matumizi ya kila senti ya fedha za maafa ya tetemeko yafuatiliwe, kila kitu kijulikane kimetumika vipi, kwa sababu haiwezekani fedha zitolewe kwa ajili ya maafa, halafu zinaishia kwenye mifuko ya mtu kwa tamaa zake," alisema.

Aidha, amebainisha kuwa michango ya maafa ya tetemeko la ardhi, ambayo iliahidiwa na bado haijatolewa, imefikia sh. bilioni 4.5 na kwamba, orodha ya walioahidi anayo, anaihifadhi.

Rais Dk. Magufuli alisema hayo jana, kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya kisasa ya sekondari Ihungo, ambapo alisema hajaridhishwa na taarifa ya ukarabati wa shule ya sekondari ya Omumwani.

Rais alisema alipouliza kuhusu gharama za ukarabati wa shule hiyo, alijulishwa kuwa zimetumika sh. milioni 116, huku kumbukumbu zake binafsi zikionyesha tayari zimetumika sh. milioni 172.8.

Papo hapo aliagiza shule hiyo ya sekondari inayomilikiwa na Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (WAZAZI), irudishwe serikalini, ambapo wanafunzi na walimu wake wote watahamishiwa serikalini.

Alisema sababu kuu ya kuchukua uamuzi huo ni ili kuiwezesha shule hiyo kupunguza changamoto zilizokuwa zikiikabili hapo awali, ambapo serikali itaweza kuiangalia kwa ukaribu.

Baadhi ya changamoto za shule hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1955, ikijulikana kama TAPA, ni uendeshaji, uchakavu wa miundombinu na uhaba wa walimu.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule sita za mkoani Kagera, ambazo zilipokea wanafunzi kutoka shule za Ihungo na Nyakato, baada ya kuharibiwa kabisa na tetemeko hilo la ardhi, lililotokea Septemba, 2016.

Kwenye hafla hiyo, ambayo pia ilishuhudiwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke, ilihudhuriwa pia na mamia ya wananchi, ambapo Dk. Magufuli alisema taratibu zote za fidia zianze kufanywa na Jumuia hiyo ya CCM ilipwe na serikali kama kuna madai yoyote.

"Ninatambua mwaka jana, kulitokea tetemeko, likasababisha maafa, ikiwemo kubomoka kwa majengo ya shule mbalimbali, ikiwemo Ihungo, makazi ya watu na miundombinu mingine.

"Shule ya Omumwani, inayomilikiwa na CCM, ilipokea baadhi ya wanafunzi wa Ihungo na kwa bahati nzuri au mbaya, mimi ndiye Mwenyekiti wa CCM, hivyo naagiza shule hiyo irudi serikalini na waziri uko hapa unasikia," alisema.

Aidha, alisema ujenzi mkubwa wa shule hiyo ya sekondari Ihungo, unafanywa kwa kutumia kiasi cha sh. bilioni sita, ambazo ni msaada kutoka Serikali ya Uingereza kupitia balozi Sarah.

Rais alisema serikali iliona vizuri kutumia fedha hizo kuijenga upya shule hiyo, ili iwe na manufaa kwa vizazi vingi vijavyo, ambapo alisema siku moja inaweza ipewe jina la Tetemeko Sekondari.

Alisema serikali haijajenga na haitamjengea mwananchi nyumba kwa sababu hakuna serikali yoyote duniani inayomjengea mwananchi nyumba baada ya maafa.

"Tuwe wakweli, serikali haitamjengea mtu nyumba. Kwenye lile tetemeko, zaidi ya nyumba 2,000 ziliharibika, serikali haiwezi kujenga nyumba zote hizo.

"Tuliahidi kutetea Watanzania wanyonge, tujipange kufanya kazi, tutahakikisha tunarudishia miundombinu ya serikali iliyoharibiwa, lakini serikali haitawajibika kujenga nyumba ya mtu mmoja mmoja," alisema.

Rais Dk. Magufuli aliongeza:"Kama unataka kuchangia tetemeko ili umchangie ndugu yako kwa ajili ya kumjengea nyumba, nenda moja kwa moja kwake usilete serikalini."

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema serikali imejipanga kuondoa kero ya makato mengi yasiyokuwa ya lazima katika mazao ya kilimo, likiwemo zao la kahawa.

Alisema lengo la serikali ni kuwaondolea wananchi mzigo mkubwa wanaobebeshwa, jambo linalowasababishia kutonuifaika na mazao yanayopatikana katika maeneo yao.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana, alipotembelea na kuweka jiwe la msingi la ukarabati wa kituo cha afya cha Kabyaile, kilichoko Ishozo wilayani Misenyi, ambacho ni miongoni mwa vilivyoathiriwa na tetemeko la ardhi.

"Mlituchagua kuinyoosha nchi kwani Watanzania wanyonge wameteseka sana, sasa ni zamu yao kufurahia matunda ya nchi yao.
Haiwezekani mwananchi wa Kagera akauza kahawa yake kwa bei ya chini, wakati nchi jirani bei iko juu huku soko la dunia ni moja.

"Sisi serikali tumejipanga kutatua changamoto hiyo hata kwenye mazao mengine tofauti na kahawa. Lazima mkulima anufaike," alisema.

Aliitaja sababu ya kushuka kwa bei ya kahawa nchini kuwa ni makato mengi yasiyo na ulazima, mfano mzuri ukiwa ni kwenye zao hilo.

"Mkulima anatozwa ushuru tofauti 30, yaani mpaka gunia nalo linalipiwa ushuru? Jamani mwanachi huyu mnyonge atabebeshwa mzigo mkubwa mpaka lini? Sasa tumedhamiria kuziondoa kodi katika zao hilo kutoka ushuru 30, angalau zibakie nne tu," alisisitiza.

Pamoja na hilo, Rais Magufuli aliagiza kikosi kazi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kinachojenga jengo hilo la zahanati, kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha linakamilika ifikapo Februari, mwaka huu, tofauti na walivyoeleza awali kuwa utakamilika Machi, mwaka huu.

"Naagiza kikosi kazi cha ujenzi cha JWTZ, kukabidhi majengo haya mapema mwezi Februari, ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili kupitia kituo chao hiki.

"Wanajeshi nawajua, kama mliweza kujenga daraja la mto Kagera usiku na mchana likaisha haraka je, hapa kinachoshindikana ni nini? Jengeni usiku na mchana ili yakamilike kwa wakati," alisema.

Rais pia aliiagiza kamati ya maafa ofisi ya waziri mkuu pamoja na kamati ya mkoa kupitia mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Salum Kijuu, kupeleka haraka fedha katika kituo hicho ili kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi huo kama alivyoagiza.

Sambamba na hilo, alimwagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kupeleka umeme wa uhakika mara moja katika kituo hicho kipya, ili kuwezesha huduma zinazotegemewa kuwepo  hasa za upasuaji, kuanza pindi kitakapokamilka.

Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika wilaya za Bukoba na Missenyi, akiwa kwenye ziara hiyo, alitoa rai kwa Watanzania kuongeza juhudi katika kufanyakazi.

Alisisitiza kuwa serikali haitakuwa tayari kutoa msaada wa chakula kwa watu wasiopenda kujituma kufanyakazi, kila mmoja kwa nafasi yake.

Pia, aliwataka wana-Kagera kutotumia maafa ya tetemeko la ardhi, kama kisingizio cha kubweteka kutofanya kazi, kwa sababu serikali yake siyo iliyotuma tetemeko liitikise Kagera.

Awali, Mkuu wa Mkoa, Salum Kijuu, alitoa taarifa fupi ya maafa ya tetemeko na kumshukuru Rais Dk. Magufuli, kwa kutembelea wahanga wa tetemeko hilo na kuwafariji.

Balozi Cooke wa Uingereza, naye alisema serikali yake imefurahishwa kwa kitendo cha serikali kutumia sh. bilioni sita walizozitoa, kwa ajili ya maafa hayo, kujenga upya sekondari ya Ihungo, ambayo ina mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya elimu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Alisema serikali yake inaunga mkono kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya 'Hapa Kazi T'u na kwamba, itaendelea kuitikia wito pale itakapohitajika kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment