Tuesday, 3 January 2017

KAMPUNI TANO ZA SIKU ZASUASUA KUUZA HISA DSE



KAMPUNI za simu za mkononi, zimesuasua kutekeleza agizo la serikali la kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Saalam (DSE), ili kuanza kuuza asilimia 25 ya hisa zao, kwa lengo la kutoa fursa kwa  Watanzania kushiriki kuzimiliki.

Hadi sasa ni kampuni tatu pekee, ndizo zilizotekeleza agizo hilo la kujisajili, huku kampuni tano zikishindwa kujiorodhesha DSE, kama zilivyotakiwa katika  marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kietroniki na Posta (EPOCA).

Kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 21(c) cha EPOCA, kampuni hizo tano, ambazo hazijatekeleza agizo hilo, zimekiuka agizo la serikali, ambalo limezitaka kampuni zote za simu kujisajili DSE na kuanza kuuza hisa kwa Watanzania.

Ofisa Masoko Mwandamizi wa DSE, Mary Kinabo, alizitaja kampuni zilizojitokeza kuwasilisha maombi ya kusajili kuwa ni Tigo, Airtel na Vodacom.

Mary alisema DSE ilipokea maombi ya kampuni hizo kutaka kujisajili Desemba, mwaka jana na kwamba, kamati ya soko hilo itapitia maombi hayo.

“Kamati itakutana ili kujadili na kutathmini kama kampuni hizo zimekidhi vigezo ili kuingia kwenye dirisha la soko kubwa au dogo,” alisema.

Mkugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi James Kilaba, alitaja idadi ya kampuni zinazopaswa kutekeleza agizo la kujisajili kwenye soko la DSE na kuuza hisa kwamba ni nane.

Kwa upande wake, Ofisa Tawala Mwandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Trano Mbarook, alisema kampuni zote za simu zinapaswa kutekeleza agizo hilo la kujisajili kwenye soko hilo la hisa.

Alisema kampuni hizo zinatakiwa kufuata sheria ya EPOCA namba 3 ya mwaka 2010, iliyofanyiwa marekebisho kupitia sheria ya fedha namba 2 ya mwaka 2016.

Desemba 27, mwaka 2016, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, aliagiza kampuni na watoa huduma wa mawasiliano, ambao leseni zao zilitolewa kabla ya Julai Mosi, mwaka jana, kujisajili katika soko la DSE katika kipindi cha miezi 6.

Agizo hilo linawataka wenye leseni za miundombinu ya mawasiliano (network facility services license), huduma za mwasiliano (network services license) na huduma za matumizi (application services license), kukamilisha taratibu za usajili kwa kuuza hisa za asilimia 25.

Mbali na hilo, kampuni zingine za simu, zilizopata leseni hizo baada ya Julai mosi, mwaka jana na kuendelea, zitatakiwa kutimiza sharti hilo la kujisajili katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu kupewa leseni.

No comments:

Post a Comment