Monday, 2 January 2017

UCHUMI WA ZANZIBAR UMEIMARIKA, MAPATO YAMEONGEZEKA



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema uchumi wa Zanzibar umezidi kuimarika, sambamba na serikali kufanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo ya kodi.

Amesema kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016, jumla ya sh. bilioni 441.3, zilikusanywa kutoka katika vyanzo vya ndani.

Dk. Shein alisema hayo juzi, katika salamu zake za kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, alizozitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Unguja.

Alisisitiza kuwa hadi kufikia robo mwaka ya pili (Aprili- Juni)
mwaka 2016, uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa kasi ya asilimia 6.2.

Dk. Shein alisema mwaka 2015, serikali ilikusanya sh. bilioni 336.6, ikiwa na maana ya miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2016, ambapo mapato yaliongezeka kwa sh. bilioni 104.7, sawa na ukuaji wa asilimia 31.1.

Alisema sambamba na mafanikio hayo, washirika wa maendeleo wamethamini kazi nzuri inayofanywa na serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi, ambapo katika kuthibitisha imani yao kwa Zanzibar, serikali ilipokea sh. bilioni 54.53, kutoka kwa washirika wa maendeleo kati ya Januari hadi Oktoba, mwaka jana.

Dk. Shein alisisitiza kuwa, huo ndio ukweli halisi na hio ndiyo hali halisi, ambayo ni vyema wananchi wakafahamu kuwa nchi ipo vizuri, kinyume na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu, ambao hawana taarifa sahihi na takwimu za uhakika za serikali.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo afya kwa kuzinduliwa majengo ya wodi mpya ya watoto na wazazi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na uzinduzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee, mkoani Pemba, baada ya kujengwa upya kwa msaada wa China.

Akizungumzia juhudi zilizochukuliwa na serikali kuwaenzi wazee, Dk. Shein alisema mwaka 2016, utekelezaji wa Pensheni ya Jamii, umeendelea kutumika, ambapo kupitia mpango huo, wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea, ambao wamesajiliwa, wameanza kupewa posho ya sh. 20,000 kwa mwezi.

Kwa mujibu wa Dk. Shein, kuanzia Aprili, 2016, utaratibu huo ulipoanza, idadi yao imeongezeka kutoka watu 21,263, waliosajiliwa mwaka 2015 hadi kufikia watu 26,603, Novemba, 2016 huku serikali ikiangalia uwezekano wa kuanza kutoa posho hiyo kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 65 hapo baadae.

Dk. Shein alisema kuwa tukio mahususi mwaka jana, lilikuwa ni kutiwa saini kwa Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016, inayoipa Zanzibar uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi.

“Hadi sasa mipango yetu katika suala hili inaendelea vizuri na tunaendelea na mazungumzo na wawekezaji mbalimbali wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa masuala ya mafuta na gesi asilia, ambao wana nia ya kuwekeza nchini kwetu,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kauli yake aliyoitoa Desemba 10, 2016, katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili, kwenye viwanja vya bustani ya Victoria ya kuwataka viongozi wa umma wanaohusika  kujaza fomu kwa kuzingatia maelekezo yaliotolewa kwenye fomu hiyo na waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli, kwani kufanya hivyo ni kuvunja maadili ya uongozi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuliwa katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani na kueleza kuwa, katika mwaka 2017, serikali itajitihidi kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo, masoko ya bidhaa zao na mafunzo na kukiendeleza kituo cha wajasiriamali kilichoko Mbweni, Unguja.

Akieleza kuhusu amani na utulivu katika kusherehekea mwaka mpya,
Dk. Shein alisema serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote au kikundi cha watu kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitemebelea Zanzibar.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kushirikiana katika kukomesha vitendo vya udhalilishaji kwani ni dhahiri kuwa, ufumbuzi wa changamoto hizo unahitaji mchango wa kila mmoja na sio serikali peke yake.

Aliendelea kutoa wito kwa wananchi, kila mmoja ajitahidi kushiriki katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, yatakayotanguliwa na shamra shamra za uzinduzi wa miradi na uwekaji wa mawe ya msingi.

No comments:

Post a Comment