Tuesday, 24 October 2017
MAKONDA AKABIDHIWA MAGARI 16 YA POLISI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekabidhiwa magari 16 kati ya 56, ya Jeshi la Polisi, ambayo yamekarabatiwa kwa msaada wa gereji ya RSA Engineering, mkoani Kilimanjaro.
Makonda, alikabidhiwa magari hayo, jana, katika hafla iliyofanyika mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema magari hayo ni salamu tosha kwa majambazi na wahalifu mkoani Dar es Salaam.
Makonda, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam, alitaja changamoto tatu zilizomsukuma kuomba msaada wa kukarabati magari hayo, ambayo yalikuwa mabovu kupindukia.
“Tukio la polisi kushambuliwa wakati wakilinda benki ya CRDB Mbande, Mbagala, wilayani Temeke, lilinifanya kuona umuhimu wa kukarabati magari haya,”alibainisha mkuu huyo wa mkoa.
Aliongeza: “Wale polisi waliuawa bila hatia, wakitekeleza majukumu yao ya kulinda fedha za wananchi. Lile lilikuwa ni funzo kwetu, hasa kutokana na aina ya magari wanayotumia kutokuwa na uwezo wa wao kujitetea kwa urahisi wakiwa ndani,”alieleza Makonda.
Tukio hilo lilitokea Agosti 23, mwaka huu, saa 1.30 jioni, wakati askari hao wakibadilishana lindo, wakiwa na gari aina ya Layland Ashock, lenye namba za usajili PT 3889.
Majambazi hayo pia yalivamia Kituo cha Polisi cha Mbande na kuchukua sare za polisi na kukimbia nazo, na pia yalipora bunduki mbili aina ya SMG .
Polisi waliopoteza maisha katika tukio hilo, E.5761 CPL Yahaya, F. 4660 CPL Hatibu, G.9524 Tito na G. 9996 PC Gastone. Pia, raia walijeruhiwa.
Makonda alitaja sababu ya pili kuwa ni tukio la mauaji ya polisi Kibiti, mkoani Pwani, Aprili 13, mwaka huu.
Katika tukio hilo lililotokea saa 12.15 jioni, Mkengeni, Kijiji cha Uchembe, Kata ya Mjawa, Tarafa na Wilaya ya Kibiti, kundi la majambazi wakiwa na silaha, walilishambulia kwa risasi gari la polisi lenye namba PT.3713, aina ya Toyota Land Cruiser na kuwaua polisi wanane.
Polisi hao ni A/INSP Peter Kigugu, F.3451 CPL Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson na H.1872 PC Zacharia. Wengine ni H.5503 PC Siwale, H.7629 PC Maswi, H.7680 PC Ayoub na kumjeruhi askari namba F. 6456 PC Fredrick.
Baada ya majambazi hao kufanya mauaji hayo, walifanikiwa kuchukua silaha tisa, kati ya hizo SMG sita, zikiwa na risasi 30 kila moja na long range tatu.
Makonda alisema matukio hayo yalichangiwa na magari, ambayo waliyokuwa wakiyatumia askari, kutokuwa rafiki ili kujibu mapigo.
Hivyo, alisema katika magari yaliyokarabatiwa, alipendekeza yabadilishwe muundo na kuwa kama ya Umoja wa Mataifa (UN), yanayotumika kulinda amani katika nchi mbalimbali duniani.
“Magari haya yameundwa katika mfumo utakaomwezesha polisi kumuona mhalifu kila upande na hata kushambulia,”alisema.
Alitaja sababu ya tatu kuwa ni kuendeleza mapambano ya vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, ambapo moja ya changamoto ni usafiri.
“Kukamilika kwa ukarabati wa magari haya ni mwendelezo wa kuhakikisha polisi mkoani Dares Salaam, wanakuwa na vitendea kazi madhubuti ili kulinda usalama na mali za raia. Tulikabidhi pikipiki za kisasa 10 na baiskeli na sasa tunakabidhi magari.
"Tunaamini yataongeza uimara wa ulinzi, hasa ikizingatiwa kuwa, Dar es Salaam ina ongezeko kubwa la idadi ya watu, ina mabalozi, wawekezaji na watu wa aina mbalimbali,”alibainisha.
Alimshukuru Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa mchango wao kuhakikisha magari hayo yanakarabatiwa.
“Pia, nawashukuru wamiliki wa gereji ya RSA, kwa kujitolea kukarabati magari haya. Hatujawalipa chochote ila ni moyo wao tu wa kuchangia maendeleo,”alisema.
Aliogeza: “Wito wangu ni kwamba, tuweze kufikiria mbinu ya kutatua changamoto, badala ya kusubiri bajeti ya serikali”.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjalo, Anna Mghwira, alimpongeza Makonda kwa ubunifu wa kufufua magari pamoja na gereji ya RSA.
“Niombe Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kuhakikisha ubunifu kama huu waliouonyesha Makonda na RSA, katika kubuni muundo wa magari haya, usitumike vibaya. Mtu akivumbua kitu chake na kikaonekana ni muhimu, tukitambue na kukithamini,”alisema.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alimshukuru Makonda kwa ukarabati wa magari hayo na kuahidi kuwa jeshi lake litayalinda .
“Tunakuahidi kuwa, mrejesho utauona. Tutahakikisha Kanda ya Dar es Salaam, inakuwa salama na hii ndiyo nia yako.Tutahakikisha magari haya yanatunzwa ili dhamira ya jiji letu kuwa salama itimie,”alisema Kamanda Mambosasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment