Tuesday 24 October 2017

LUKUVI AAGIZA NYUMBA ZILIZOJENGWA HOLELA ZIVUNJWE



SERIKALI imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Maofisa Ardhi, Ujenzi na Mipango Miji, kuweka alama za X na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali.

Pia, wametakiwa kuvunja majengo yote yaliyojengwa katika viwanja vilivyopewa hati miliki za ardhi kwa dhuluma.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi.

Aliagiza eneo lililokuwa shamba la mifugo la Malonje, wilayani Sumbawanga, lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa ulikiukwa kwa kiwango kikubwa na masharti ya uendeshaji hayakuzingatiwa.

Waziri Lukuvi alisema, tatizo la ujenzi holela linaanza pale ambapo wakurugenzi watendaji wa halmashauri, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji, wanapoacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndiye anayejenga.

“Hatuwezi kuendelea na kazi ya kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana. Kwa hiyo naagiza kuweka X katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa dhuluma," alisema.

Lukuvi alisema atapambana na viongozi pale ambapo atakuta majengo yamekithiri katika miji yao na hayana vibali vya ujenzi na yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.

Katika hatua nyingine, Lukuvi alisema serikali inakusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi, lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.

Alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa, kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi, lakini wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, Dubai na kwingine duniani.

Lukuvi alisema haiwezekani mtu atumie ardhi ya Tanzania kujipatia fedha, halafu azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi kama pori, jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.

“Kwa hiyo wizara yangu imekusudia mwezi ujao, kupeleka bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka 1999, ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana," alisema.

Alisema kuanzia Novemba, mwaka huu, tatizo hilo litakwisha kwa kuwa jukumu hilo zitapewa benki na wakopeshaji wote, ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo, kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika benki husika.

“Na kama benki husika haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi serikali itamyang’anya mkopeshwaji huyo shamba hilo, kwa kuwa atakuwa amekiuka sheria, halafu benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleze shamba lile, itakuwa imekula hasara," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kamishna mstaafu Zelotte Stephen, alimhakikishia Waziri Lukuvi kuwa, atayafanyia kazi mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.

No comments:

Post a Comment