KINARA
wa mtandao wa biashara za dawa za kulevya, Kambi Zubeir Seif, maarufu kwa jina
la Cambiasso, ametiwa mbaroni, kufuatia msako mkali uliofanywa na Polisi Kikosi
Maalumu cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, katika nyumba yake ya
kifahari aliyokuwa amejificha iliyoko Tuangoma, wilayani Kigamboni, Dar es
Salaam.
Cambiasso,
pia inadaiwa mwaka 2011, alikamatwa na kilo 179, za dawa za kulevya aina ya
heroine, akiwa na wenzake watatu, Fredy Chonde, ambaye ni Mtanzania, Muhammad
Shahbaz na Abdulghan Gulam, ambao ni raia wa Pakistan.
Mfanyabiashara
huyo anayemiliki nyumba za kifahari pamoja na magari, anayedawa kuwa kinara
muunganishaji wa mitandao ya dawa za kulevya, alikamatwa usiku wa kuamkia
Desemba 10, mwaka huu, katika operesheni kali ya kuwasaka wafanyabiashara wa
dawa za kulevya nchini.
Wengine
waliokamatwa kwenye msako huo ni Marashi Zuberi Seif, ambaye ni dada wa
mtuhumiwa namba moja na rafiki wa kike wa Cambiasso, Grace Aseasisye, ambaye
alipangiwa nyumba eneo la Yombo Buza.
Imeelezwa
kuwa polisi inaendelea na msako mkali baada ya watuhumiwa wengine kukimbia,
ambapo kwa mujibu wa chanzo chetu, operesheni hiyo ni mwanzo wa operesheni
kubwa zitakazoendeshwa na polisi kuumaliza mtandao huo unaohatarisha nguvu kazi
ya vijana.
Akizungumzia
kukamatwa kwa kinara huyo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha
Kuzuia na Kupambana na Dawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Mwandamizi Msaidizi
wa Polisi (SACP), Mihayo Msikhela, alisema Cambiasso alikamatwa
Ijumaa, iliyopita na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
“Huyu ni kiunganishi wa mitandao hiyo.
Polisi walifanikiwa kumtia nguvuni baada ya kuweka mtego nyumbani kwake na Ijumaa
alishafikishwa mahakamani kujibu moja ya kesi inayomkabili,” alisema Kamanda
Msikhela.
Kwenye
kesi hiyo, mtuhumiwa huyo aliunganishwa katika kesi namba PI 23/2016 ya raia wa
Nigeria, Bede Eke, aliyekamatwa Juni, mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, akiwa na kilo tano za dawa za
kulevya.
Anakabiliwa
na kosa la kula njama (conspiracy) na kusafirisha dawa za kulevya pamoja na
raia huyo wa Nigeria.
Msako
huo ni hatua za mapambano dhidi ya mtandao huo, ambao serikali ya awamu ya tano
imeahidi kuutokomeza.
Katika
mkesha wa kuliombea Taifa, Desemba 31, mwaka jana, Rais Dk. John Mafuguli,
alisema Taifa kwa kipindi kirefu lilikabiliwa na vigogo wauza dawa za kulevya,
watumishi na vigogo wakwepaji wa kodi pamoja na wizi wa dawa hospitalini, hivyo
viongozi wa dini na Watanzania wote wanapaswa kumuombea ili aweze kutumbua
majipu ya mafisadi hao.
Dk.
Magufuli, ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi, alisema viongozi wa dini wanapaswa kuendelea
kuliombea Taifa na kuwaombea watu wabaya wasiopenda maendeleo waweze kubadilika
ili nchi iweze kusonga mbele.
“Viongozi
wa dini tunapaswa kuendelea kumuombea rais wetu (Dk.Magufuli), aendelee
kutumbua majipu haya, ambayo yanasababisha maendeleo ya Taifa letu kurudi nyuma,”
alisema Lukuvi.
No comments:
Post a Comment