RAIS Dk. John Magufuli, amefanya uteuzi wa wakuu wa wilaya wawili na wakurugenzi watatu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi, Dar es Salaam, jana, imeeleza kuwa, Rais Dk. Magufuli amemteua Kisare Makori kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo.
Makori anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Humphrey Polepole, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi.
Rais Dk. Magufuli pia, amemteua Avod Herman kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, iliyoko mkoani Mtwara.
Herman anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Khatib Kazungu, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Aidha, Rais amemteua Ramadhan Mwangulumbi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, iliyoko mkoani Shinyanga.
Mwangulumbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Lewis Kalinjuna, ambaye anastaafu kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli amemteua Rojas Romuli, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Romuli, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ngalinda Ahmada, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Rais Magufuli pia, amemteua Rashid Gembe, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Gembe, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mkumbo Barnabas, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, uteuzi huo unaanza mara moja na wateule wote wanatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), mara wapatapo taarifa.
No comments:
Post a Comment