Tuesday 18 April 2017

MADUDU ZAIDI YABAINIKA WETCU, GARI LA MWAKA 2008 LANUNULIWA KWA MIL. 220/-


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema timu aliyoiunda kuchunguza tuhuma za ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU), imekamilisha kazi yake, ambapo imebaini madudu mengi zaidi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi, mkoani Tabora, wakati akizungumza na wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa wadau wa zao la tumbaku, kwenye ukumbi wa Kiyungi Mwana Isike.

“Nilikuja Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo (juzi) nimekuja kuendelea na mkakati wa serikali ya awamu ya tano wa kuwezesha kilimo cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima, wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na viongozi wa serikali wawepo kwenye mkutano huu,” alisema.

Akitoa mrejesho juu ya uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda, Waziri Mkuu Majaliwa alisema, WETCU haikuwa na kitengo cha ununuzi kwa zabuni kwani waliunda kampuni ya FDTU (Flu and Dark Tobacco Union), ambayo ni Umoja wa Wenyeviti wa Muungano wa Vyama vyote vya Tumbaku.

Majaliwa alisema kampuni hiyo ilipewa jukumu la ununuzi wa pembejeo, lakini walikuwa wanagawana fedha.

“Tumefanya ufuatiliaji hadi kwenye akaunti za benki, lakini hakuna fedha mpaka sasa. Tumeangalia chanzo cha fedha za Union zenu na kubaini hakuna fedha zinazotoka FDTU kwenda WETCU,” alisema.

Akifafanua kuhusu kashfa ya ununuzi wa gari aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili T181 DEN, ambao ulifanywa kinyume na maazimio ya mkutano mkuu, Waziri Mkuu alisema viongozi wa WETCU walitumia zaidi ya sh. milioni 220, kuzidi kiwango kilichoidhinishwa na mkutano mkuu cha kununua gari lenye thamani ya sh. milioni 40.

“Gari walilolinunua ni la mwaka 2008 na siyo la mwaka 2015, kama taarifa zinavyoonesha. Lilikwishatumika kwa kilometa zaidi ya 95,000, lakini likarekebishwa hadi kubakiza kilometa 16,000, ili lionekane ni jipya.

“Maana yake wamekula fedha nyingi sana na ni lazima tuwachukulie hatua za kisheria kwa sababu wamekula fedha, wamenunua gari lililotumika na siyo maamuzi ya mkutano mkuu,” alisisitiza.

Waziri Mkuu aliagiza Mkurugenzi wa Kampuni ya 4x4 Tanzania Limited, Faraz Yaseen, akamatwe na kuhojiwa kwa nini alihusika kuuza gari la mwaka 2008, lakini akabadilisha nyaraka ili lionekane ni la mwaka 2015.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uuzaji wa hisa za WETCU, Waziri Mkuu alisema chama hicho kilikuwa na hisa milioni 36, ambapo kilitoa hisa milioni sita ili ziuzwe na zikapatikana sh. bilioni 2.5.

“Walichukua hisa 100,000 na kuziuza na wakapata sh. milioni 250, lakini fedha hizo hazikuwekwa kwenye akaunti ya chama. Hisa zilizobakia ambazo ni milioni 30, walishaanza mchakato wa kuuza hisa milioni 28.

“Kwa vile hawakupata idhini ya mkutano mkuu na wala hawakufuata taratibu, kanuni na sheria, kuanzia leo (juzi) nimesitisha mauzo ya hisa hizo. Mrajisi fuatilia Zani Security warudishe kile cheti kinachowapa dhamana ya kuuza hizo hisa,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwa vile WETCU ina madeni mengi katika Benki za CRDB na NMB, viongozi wa chama hicho waliamua kufungua akaunti mpya za fedha za Kitanzania na dola kwenye benki ya EXIM.

Aidha, alisema walifungua akaunti ya muda maalumu na kuweka fedha ambazo zilizalisha faida ya zaidi ya sh. milioni 14, katika kipindi cha miezi mitatu.

“Ninamuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kupitia COASCO (Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika), afuatilie benki ya EXIM hapa Tabora ili kubaini ni kinanani walikuwa wakifanya miamala hiyo,” alisema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za mkoa huo.

Machi 16, mwaka huu, Waziri Mkuu aliivunja Bodi ya WETCU na Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo na kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Pia, alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, awakamate viongozi wanne  na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment