Thursday 20 April 2017

MAGUFULI ATOA AJIRA KWA MADAKTARI 258


RAIS Dk. John Mafuguli ameagiza kuajiriwa mara moja madaktari 258 na wataalam wengine 11 wa afya, waliojitokeza na kukidhi vigezo katika mchakato wa kuomba ajira nchini Kenya.

Dk. Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umekuja baada ya baadhi ya madaktari nchini Kenya, kuwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka serikali ya nchi yao kusitisha ajira za madaktari 500, kutoka Tanzania ambao waliombwa na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

Waziri Ummy, alitoa kauli hiyo bungeni mjini hapa jana, wakati akizungumza na wandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge.

Ummy alisema kufuatia uamuzi huo, majina ya madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi, yatatangazwa kupitia tovuti ya wizara hiyo.

"Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za madaktari ilikubalika na pande zote mbili (Tanzania na Kenya), kuwa iwe imekamilika ifikapo Aprili 6, mwaka huu na kwamba, madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya, kati ya Aprili 6-10, mwaka huu, na kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za madaktari wa Tanzania nchini Kenya, Rais Dk. Magufuli, amefikia uamuzi kwamba, madaktari wote 258, ambao walikuwa tayari kwenda kufanyakazi nchini Kenya, waajiriwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara moja.

“Rais alinipigia simu jana, akaniuliza, uliniambia kuwa madaktari wanatakiwa kuondoka tarehe 10, leo ni tarehe ngapi? Sasa mimi sio mtu wa maneno ni mtu wa vitendo, naagiza madaktari hao wote 258, waajiriwe hapa nchini mara moja. Tunampongeza na kumshukuru sana kwa uamuzi wake huo,” alisema Waziri Ummy.

Waziri huyo alisema Machi 18, mwaka huu, wizara yake ilitangaza nafasi hizo, ambapo hadi kufikia Machi 27, mwaka huu, jumla ya maombi 496, yaliwasilishwa na baada ya kufanyiwa uchambuzi, ilibainika kuwa madaktari 258 walikuwa wamekidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanyakazi nchini Kenya.

"Baadhi ya vigezo vilivyotakiwa vilikuwa ni pamoja na vyeti vya taaluma na vyeti vya sekondari, chuo alichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo, sehemu alipofanya mafunzo kwa vitendo na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo na uzoefu wa kazi," alisema.

Alivitaja vigezo vingine kuwa umri wa mwombaji usiozidi umri wa miaka 55, usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika na asiwe mtumishi wa umma, hospitali teule za halmashauri na hospitali za mashirika ya hiari wanaolipwa mishahara na serikali.

Waziri Ummy alisema wakati serikali ikiwa katika mchakato wa kukamilisha utaratibu wa ajira za madaktari wake nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa maombi ya kazi, kuandaa hati ya makubaliano kati ya Serikali a Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo, madaktari watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi  mahakamani kuitaka serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri madaktari kutoka Tanzania.

Alisema kimsingi Tanzania inakabiliwa na uhaba wa madaktari, lakini changamoto waliyo nayo ni rasilimali fedha.

No comments:

Post a Comment