Thursday, 20 April 2017

SPIKA NDUGAI AAGIZA HOTUBA ZA UPINZANI BUNGENI ZIFUATILIWE



SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amewaagiza makatibu mezani, kufuatilia hotuba za kambi rasmi ya upinzani bungeni ili kubaini watu wanaoziandika kutokana na aina ya maneno yanayotumika katika hotuba hizo.

Ndugai alitoa alitoa kauli hiyo bungeni jana, wakati kambi ya upinzani ilipokuwa ikiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Umma na Utawala Bora.

Katika hotuba hiyo iliyosomwa na Ruth Molel, Spika Ndugai aliagiza
kuondolewa kwa maneno, ambayo yalikuwa yakimshutumu yeye moja kwa moja.

Ndugai alisema Bunge la Tanzania linatumia utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Ulaya katika uendeshaji wa shughuli zake, hivyo ni makosa kumlaumu Spika moja kwa moja.

"Tunafanya vitu kwa kwa utamaduni, kumlaumu Spika kwa vitu vya aina hii na moja kwa moja, lazima taarifa hii haiandikwi na mbunge, kuna mtu anawaandikia huko.

"Hata sielewi, ambaye hajui taratibu hizi, hatufanyi hivyo. Huwezi kuwa mahakamani pale, wewe ni hakimu, halafu unamtuhumu jaji, yaani mimi ni kiongozi wenu nyinyi, mnavyokuwa mnaniwekea maneno ya ajabu, sijui kama ni sahihi,"alisema.

Ndugai alisema kwa mtindo huo, kamwe chombo hicho hakiwezi kuheshimika kwani kufanya hivyo ni kukivunjia heshima.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, haelewi kama hayo maneno ni ya lazima kuandikwa kwenye hotuba hizo.

Spika Ndugai alihoji ni mbunge yupi aliyepeleka taarifa ofisini kwake kwa maandishi ama kwa mdomo kuwa, ametishiwa maisha kwa kuwa hajawahi kumuona mtu yeyote akifanya hivyo.

"Aliyesema kwamba ametishiwa maisha, labda anataka kuuawa. Niwaulize nyie wabunge, aliyeniletea taarifa ama kwa kuniambia au kuniandikia kwamba mimi mbunge wako natishiwa maisha jina lake nani?" Alihoji.

"Kwa hiyo vitu vingine sio vya lazima, Bashe yupo hapa, je umewahi kumuona Spika na kumwambia chochote? Haya nitajieni nyie hao waliotishiwa,"alisema.

Alitaka kujua kama umefika wakati, ambao mbunge yeyote akisema hapo ndani ametishiwa maisha, bunge zima linakwenda na upepo.

Kuhusu kuwadhibiti wabunge wa upinzani kutoa mawazo yao kwa uhuru, Ndugai alisema hakuna mbunge yeyote anayedhibitiwa kuzungumza wala kutoa maoni yake na kwamba, kila mtu ana uhuru wa kutosha.

"Hivi kwanini mnajiweka kwenye hali fulani ya kuona kwamba unaonewa?
Hivi unaonewa na nani? Kanuni ni za wote, taratibu ni za wote, hakuna mtu aliyethibitiwa chochote,"alisema Ndugai.

Alifafanua kuwa, katika bunge hilo, kila mtu anatoa mawazo yake kwa uhuru wake, hivyo anashangaa kusikia watu wanasema wananyimwa uhuru wa kuzungumza.

Akizungumzia kuhusu kuingilia mhimili wa mahakama, Ndugai alisema, wanatumia sentensi, ambazo sio nzuri katika hotuba zao na mahakama ni chombo chenye heshima yake.

Wakati Spika Ndugai akiendelea kutoa ufafanuzi huo, wabunge wa kambi ya upinzani waliendelea kutoa maneno mbalimbali ya kuudhi, hali iliyomfanya aendelee kuwaonya.

No comments:

Post a Comment