Thursday, 20 April 2017

WABUNGE WATAKA POSHO ZA MADIWANI ZIONGEZWEWABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wameitaka serikali kuongeza posho za madiwani kutokana na wawakilishi hao wa wananchi kufanyakazi nyingi, zikiwemo za kusimamia fedha za miradi, inayopelekwa kwenye halmashauri zao.

Walitoa kilio hicho bungeni mjini hapa jana, wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.

Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje (CCM), alisema posho wanazolipwa
madiwani ni kidogo, ikilinganishwa na kazi wanazofanya kwenye halmashauri, ikiwemo kupitisha fedha za miradi mikubwa ya kusaidia maendeleo ya wananchi.

Lubeleje, ambaye ni miongoni mwa wabunge wakongwe nchini, alisema posho wanazopata madiwani ni zile zilizopitishwa mwaka 2012 na tangu hapo hawajaongezewa tena kwa kipindi cha miaka mitano sasa.

Aliitaka serikali iwaingize kwenye kundi la wafanyakazi wa serikali wa mikataba, ili wanapomaliza kipindi chao cha miaka mitano, wapewe mafao au kiinua mgongo kama wanavyofanyiwa viongozi wengine, wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya.

Mbunge huyo alisema viongozi hao waliingizwa kwenye mfumo wa kulipwa mafao baada ya miaka mitano, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba mwaka 1999, hivyo ni vema madiwani nao wakafikiriwa kuingizwa katika mfumo huo ili wapate kiinua mgongo wakistaafu.

Alisema amekuwa diwani kwa miaka 15 na mwenyekiti wa halmashauri kwa miaka 15, anajua ugumu wa kazi za madiwani, hasa wakati huu, ambao pamoja na kuhudhuria vikao, pia wamekuwa na majukumu mazito ya kusimamia na kufuatilia fedha zinazoingizwa kwenye miradi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Felista Bura (CCM), alisema serikali inatakiwa kuwalipa posho madiwani ambao wamekuwa wakifanyakazi kubwa ya kusimamia miradi ya fedha nyingi za serikali.

“Madiwani wanafanyakazi kubwa kwenye halmashauri, wanatakiwa kuongezewa posho kutokana na kuwa na jukumu la kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo. Wakati umefika, wanatakiwa kukumbukwa na kuongezewa posho zao,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sevelina Mwijage (CUF), alisema serikali imekuwa ikiwakopa madiwani kutokana na kutowalipa posho zao wakati wakifanya vikao vya kupitisha miradi katika halmashauri mbalimbali nchini.

Pia, aliiomba serikali kuharakisha kupeleka bungeni mswada unaoagiza kupitishwa kwa sheria ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Akizungumzia sekta ya ualimu, alisema mazingira yaliyoko katika ualimu yanasikitisha, shuleni hakuna vyoo, maji hakuna hivyo alitaka yaboreshwe.

“Tunasomesha vijana wetu, lakini wakimaliza hawana ajira, wana vyeti vizuri tu, lakini wanaendesha bodaboda, tuwape ajira watoto wetu ili wafaidi elimu iliyopo,” alisema Mwijage.

Kuhusu sekta ya Afya alisema Bukoba mjini hakuna chumba cha kuhifadhi maiti, hatuna wodi ya wanawake, hivyo serikali inapaswa kuwa inafanya vitu vinavyoeleweka, sasa kuna vitanda wiwili tu,

Mbunge wa Viti Maalumu, Anjelina Malembeka (CCM), aliomba serikali kuongeza posho za madiwani, ambazo hazijaongezeka kwa muda mrefu kutokana na kazi kubwa wanazofanya kuongezeka kwenye halmashauri zao.

Mbunge wa Nanyumbu, William Nkurua (CCM), alisema wakati umefika kwa serikali kuwaongezea posho madiwani, ambao wamekuwa wakisimamia miradi ya wananchi.

Alisema katika utaratibu wa kawaida, madiwani wanalipwa posho ya kila mwezi sh. 350,000, posho za vikao kuanzia sh. 100,000 hadi 500,000, kiwango ambacho kinapishana kutoka halmashauri moja hadi nyingine.

Mbunge wa Mchinga (CUF), Amidu Bobale, alisema hatua ya usalama wa Taifa kuanza kuwashughulikia wabunge, ni kulishusha hadhi bunge.

Alisema  maongezi yanayoongelewa bungeni kwa mujibu wa katiba ya nchi hayapaswa kuhojiwa kokote.

Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Upendo Peneza, alisema suala la utawala bora, uwazi na uwajibikaji ni la msingi na kwamba, miaka ya nyuma wananchi wameshirikiana na wabunge kuiwajibisha serikali tofauti na utawala wa sasa.

No comments:

Post a Comment