Friday, 21 April 2017

MAKOMANDOO KUPAMBA GWARIDE LA MUUNGANONa: Lilian Lundo – MAELEZO

Kikosi cha Makomandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kitapamba maadhimisho ya  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayoadhimishwa  Aprili 26, mwaka huu  Mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu Jenista Mhagama  maadhimisho hayo yatafanyika katika uwanja wa Jamhuri  Mjini  Dodoma ambapo mgeni Rasmi atakuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Taarifa ya  Waziri Mhagama ameteja shughuli  zinazotarajiwa kufanyika siku ya Muungano  kuwa ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama (JWTZ,JKT, Polisi na Magereza), maonyesho ya kikosi cha Makomandoo, onesho la Mbwa na Farasi waliofunzwa.

Aidha, Mhagama aliongeza kuwa mambo mengine yatakayofanyika ni gwaride la uzalendo la wanafunzi wa shule za sekondari za Dodoma,  burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka Dodoma na Zanzibar Yamoto Band, Mchungaji Zayumba, Jacob Beats, Mwenge Jazz Band na Mgosi Maturumbeta.

“Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka  53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na Kuumarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,” alifafanua Jenista Mhagama.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo muhimu kwa kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya nchi.

“Ninaomba kuchukua nafasi ya pekee kuwaomba wananchi wote waliopo Dodoma kujitokeza kwa wingi  uwanja wa  Jamhuri siku hiyo ya Jumatano  tarehe  26 Aprili  2017 kuanzia saa 12:00 asubuhi ili kusherehekea kwa pamoja maadhimisho hayo muhimu kwa nchi yetu,” alisema Jenista Mhagama.

Maadhimisho ya Muungano yanafanyika kwa mara ya kwanza Mjini Dodoma  Tangu Taifa Letu lipate uhuru na kutangazwa kuwa Makao Makuu. 

No comments:

Post a Comment