Tuesday 18 April 2017

VIONGOZI WA DINI WAKEMEA UHALIFU, MAUAJI YA POLISI


WATANZANIA wametakiwa kuchochea umoja na amani ili uendelee kuwepo nchini, kutokana na kuwepo kwa viashiria vinavyotishia kutoweka kwa utulivu.

Pia, wametakiwa kubadilika kifikra na kutokuwa mstari wa mbele katika kuwatishia Watanzania wenzao kwa kufanya uhalifu.

"Tukiwa tunakwenda kuadhimisha miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika, kitaifa tuna mambo mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Tuna umoja, ambao umeipatia nchi jina la amani," alisema Muashama Baba Askofu Dk. Isaac Amani na kuwataka Watanzania kujenga nchi kwa uzalendo kwa ajili ya maendeleo kwa wote.

Dk. Amani aliyasema hayo jana, wakati wa Ibada ya Sikuu ya Pasaka Kitaifa, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi.

"Umoja na amani ni kama moto unaotakiwa kuchochewa ili kuendelea kuwaka kwani usipochochea utazimika. Kitaifa tunaathirika na mambo mengi yanayorudisha nyuma maendeleo, yakiwemo ulevi wa pombe na dawa za kulevya," alisema Dk. Amani na kusisitiza kuwa, hatima ya Tanzania iko mikononi mwa Watanzania wote.

Alisema wananchi wengi wanakosa mipango na malengo, jambo ambalo ni hatari sana kwa kuwa muda unapotea huku siku zikisonga mbele.

Dk. Amani alisema kutokana na hilo, wananchi wengi wanapoteza rasilimali muda na kutumia fedha kwenye mipango ya ovyo kwa ulevi, kuhonga na kupenda anasa.

Aidha, alisema binadamu wenyewe kwa wenyewe wanaingia katika vita kwa kugeukana, kudanganyana na kutumiana kama sehemu ya kujipatia kipato.

Pia, alisema kuna wengine wamejiingiza kwenye ugaidi ili walipwe, utapeli na dhuruma,  hivyo alionya  haiwezekani furaha ya Injili kupatikana kwa aina hiyo.

"Matendo ya ubakaji na ulawiti yapo waziwazi kabisa, matendo ya aibu yanahusishwa na utandawazi. Tunasoma na kuyabeba na kuyafanyia kazi katika jamii. Tutumie elimu na mafundisho katika kujifunza yale yaliyo mazuri," alisema.

Mbali na hayo, aliwasihi wananchi kuzingatia kanuni za afya na kutopeana hofu na msongo wa mawazo katika familia kwa kuwa maradhi mengine ni ya kujitakia.

Aliwataka wananchi kukata bima za afya kutokana na umuhimu wake, kwa kuwa bila ya kuwa na kadi hizo, gharama za matibabu ni kubwa mno, jambo ambalo husababisha wengine kupoteza maisha kutokana na kushindwa kumudu gharama.

Dk. Amani aliwasihi wananchi waliokata kadi hizo, kuzitumia ipasavyo kwa kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa afya zao, badala ya kusubiri mpaka wazidiwe na kwa wagonjwa, kuzingatia unywaji wa dawa kwa wakati na kuacha kuendekeza mambo yatakayowafanya kukatiza dozi.

Alitaka kuwe na malengo makubwa ya kushirikiana na mataifa mengine katika nyanja mbalimbali.

Dk. Amani aliwataka wanasiasa watumie nguvu katika maendeleo ya nchi kwa ujumla, badala ya kuweka mbele vyama vyao.

Kuhusu mauaji ya vikongwe na albino, Dk. Amani alisema kuna vitendo ambavyo vimekuwa tishio la usalama kwa watu hao, ambapo watoto wenye ualbino wamefichwa katika kambi kutokana na jamii kuwawinda.

"Viungo vya albino na vikongwe kuuawa ni matendo vinavyoshangaza ulimwengu. Wazee wetu, babu zetu wanaishi kwa hofu. Watoto albino wamefichwa katika kambi kutokana na jamii inawawinda. Tumekuwa tishio la usalama wa baadhi ya wenzetu," alisisitiza Dk. Amani na kueleza kushangazwa na matukio ya upoteaji wa watoto.
 

AKERWA WANAOFURAHIA MAUAJI YA ASKARI

Dk. Amani pia alikemea tabia mbaya, iliyoibuka hivi karibuni ya baadhi ya wananchi kufurahia mauaji ya polisi

"Tuchochee amani. Majambazi yameangamiza wananchi wengi barabarani, nyumbani sasa askari wanane, hii ni mbaya sana. Ajabu kubwa wapo wananchi wanafurahia na kushangilia, tumefika huko!" Alihoji Dk. Amani na kusema kwamba, unahitajika msaada wa Mwenyezi Mungu kufikiria na kubadilika kwa kuwa hali siyo nzuri.

"Mambo yanayotishia umoja na amani yapo katika fikra. Tunaotishia ni sisi wenyewe kwani uhalifu unaanzia katika fikra, unaishia kwenye vitendo," alisema.

AONYA SIASA ZA CHUKI

Dk. Amani alisema kuna wanasiasa badala ya kufanya siasa safi, wamekuwa wakiingiza chuki binafsi na ubinafsi, vitu ambavyo vinadhoofisha taifa.

Kutokana na hayo, aliwataka Watanzania, serikali na viongozi, kulaani vitendo vyote vya uhalifu, ambavyo vinataka kuliingiza taifa kwenye kaburi. 

Aliwataka waombe nchi iwe na umoja ili sura na hadhi ya Tanzania viendelee kuwepo kwa kuwa hatima ya Tanzania iko mikononi ma Watanzania wote.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth, jana waliungana na waumini wa Kanisa la Africa  Inland– Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni, kusali Ibada ya Sikukuu ya Pasaka.

Katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba Askofu Charles Salalah, aliongoza maombi ya kumuombea Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na alimpongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini, ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali za umma.

“Rais unafanyakazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua wewe ni majipu madogo madogo yaliyotokana na jipu kuu, ambalo ni dhambi za mwanadamu na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu. Kwa hiyo sisi Wakristo wenzako na waumini wengine, tunakuombea sana na tunakuunga mkono katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogo madogo ya watumishi hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi,” alisema Askofu Salalah.

Akizungumza katika Ibada hiyo, Rais Magufuli aliwashukuru Wakristo wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee. Pia, amewataka waiombee nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.

Mapema asubuhi, Rais Magufuli alishiriki Ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro, lililoko katika Parokia ya Oysterbay, Jijini Dar es Salaam, ambapo katika salamu zake za Pasaka, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alisema baraka zilizoletwa na Yesu Kristo aliyefufuka ni kwa ajili ya watu wote wakristo na wasio wakristo.

Alisema yeye na kanisa  wanamtakia heri Rais Magufuli ili matumaini ya baraka hizo ziwafikie Watanzania wote, pamoja na kumtaka kuwa imara katika changamoto na machungu anayokutana nayo katika uongozi huku akimwambia: “Yesu Kritso akuimarishe na akutie nguvu ili matumaini tunayoyadhimisha leo yawafikie Watanzania wote.”

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Nathaniel Limu, anaripoti kutoka Singida kuwa, Askofu mstaafu wa Kanisa la Pentekoste (FPCT), mjini humo, Dk.Paulo Samweli, ametoa rai kwa madhehebu ya dini nchini, kuliombea taifa liweze kuondokana na umwagaji wa damu kwa Watanzania wasio na hatia, wakiwemo askari polisi.

Dk. Paulo amesema mauaji ya polisi wanane, yaliyofanyika Kibiti mkoani Pwani hivi karibuni, hayavumiliki kabisa na kila Mtanzania anapaswa kuyakemea na kuhakikisha mauajio hayo hayajirudii tena.

Alisema madhehebu ya dini na Watanzania kwa ujumla, waungane kulaani na kukemea vikali mauaji hayo ya kinyama, ambayo yamekatisha uhai wa askari polisi wakati wakilitumikia taifa.

Dk. Paulo alisema jukumu la askari polisi ni kulinda Watanzania wa madhehebu ya dini, wasio na dini na mali zao.

"Sasa walinzi wetu hawa na mali zetu,. tena wasiokuwa na hatia yoyote, wanauliwa inakuaje? Tukianza kuwaua kwa ukatili namna hii, nani atatulinda.Wewe ukimuua askari polisi, ujue wazi kuwa unajiua mwenyewe bila ya kujijua. Unyama huu haukubaliki mbele ya Mungu na kwa Watanzania wote wema. Tuungane kuukomesha," alisema.

Dk. Paulo alisema madhehebu ya dini yote bila kujali itikadi zao, yaungane kufanya maombi maalumu ili mauaji haya yasifanyike tena hapa nchini huku shughuli za wananchi zikisimama kutokana na wananchi kuingiwa na hofu.

"Tusipofanya maombi kwa Mwenyezi Mungu kwa umoja wetu,vitendo hivi zinaweza kusambaa sehemu mbalimbali ya nchi yetu. Tukifika huko, Tanzania yetu inayosifika kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu, haitakalika tena,"alisema.

Dk.Paulo alisema shughuli za kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa uhuru mpana kama ilivyo hivi sasa, zitakuwa ngumu mno, kujiletea maendeleo nako kutakuwa ni shida kutokana na uwepo wa viasharia vya ufunjifu wa amani.

Wakati huo huo, wananchi wametakiwa kushirikiana na serikali kukemea na kukomesha vitendo vinavyodhalilisha utu, ikiwemo mauaji ya kutisha, kutekwa nyara, ufisadi, uzembe wa baadhi ya watumishi, dawa za kulevya na kukosekana kwa haki.

Aidha, ongezeko la matendo hayo limetajwa kuwa ni dalili za watu kutokuwa na imani ya kweli, hivyo ni vyema kusimama kuomba na kulaani matendo hayo ya uovu yanayoliingiza Taifa katika kaburi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padre Raymond Sabba, alisema hayo juzi, katika mkesha wa Ibada ya Pasaka, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Alisema ni muhimu mambo ya uovu yanayodhalilisha utu wa Mtanzania,  kukemewa na wananchi kuhakikisha wanaliombea taifa katika kipindi kigumu kilichopo ili kudumisha amani.

“Matendo ya mauaji ya kutisha, watu kutekwa nyara, ufisadi, uzembe wa watumishi, dawa za kulevya na kukosekana kwa haki, sio vitendo vya kumpendeza Mungu, ni makaburi, hivyo Taifa tushirikiane katika maombi ili kuondokana na hali hiyo,”alisema.

Alisema matendo hayo si kwamba yanafanywa na watu, ambao hawana dini  bali wengi wao ni waumini wazuri, ikiwemo Wakristo Wakatoliki, ambao wanajitanabaisha kwa Kristo kwamba, ni Wakristo wakati wanatenda matendo yasiyofaa.

Alisema hatua ya nchi kupitia katika matukio ya kutisha, ikiwemo  mauaji ya ajabu kwa watu wasio na hatia, wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe na kukosekana kwa haki kwa wanyonge, ni kumkosea Mungu, hivyo kila mmoja kwa imani yake, asimame kuomba ili kudumisha umoja, ushirikiano, utu na uzalendo uweze kubaki moyoni.

No comments:

Post a Comment