MAJAMBAZI wanne wanaodaiwa kushiriki katika tukio la mauaji ya
askari wanane, ambao waliporwa silaha saba, zikiwemo aina ya SMG, katika maeneo
ya Mkengeni wilayani Kibiti, mkoani Pwani, wameuawa huku silaha nne
zikipatikana, zikiwemo mbili zilizoibwa kwa askari hao.
Kutokana na mwendelezo wa matukio ya ujambazi katika eneo
hilo, Jeshi la Polisi nchini, limesema linakwenda katika operesheni ya moto, ambayo
haina mwisho, hivyo kuanzia sasa eneo hilo la tukio, Mkuranga, Kibiti na Rufiji
marufuku kuendesha pikipiki zaidi ya saa 11 jioni.
Wakati jeshi hilo likitoa taarifa hiyo jana, Rais Dk. John
Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini,
Ernest Mangu na kuwataka Watanzania wote kutoa ushirikiano ili kukomesha
vitendo vya kuwashambulia polisi, ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya
kulinda raia na mali zao.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato
Marijani, alisema majambazi hao waliuawa kutokana na hatua za kiintelejensia na
kiupelelezi, zilizochukuliwa, ambapo askari waliweza kufuatilia na kubaini
maficho yao ya muda baada ya kuwaua
wenzao waliokuwa wakitoka lindo.
“Katika majibizano ya
risasi kati ya polisi na watuhumiwa hao,
majambazi wanne waliuawa na bunduki nne kupatikana, mbili zikiwa
zilizoibwa katika tukio la Mkengeni na nyingine mali za majambazi hao,” alisema
Kamishna Marijani, wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo kutokana na mauaji ya
askari hao wanane.
Kamishna Marijani aliwataja askari waliofariki katika tukio
hilo, wakiwa wanatoka kubadilishana lindo na kupigwa risasi katika barabara ya
Dar es Salaam- Lindi kuwa ni Mrakibu Msaidizi Peter Kigugu, F. 3451 CPL
Francis, F. 6990 PC Haruna, G. 3247 PC Jackson, H. 1872 PC Zacharia, H. 5503 PC
Siwale, H. 7629 PC Maswi na H. 7680 PC Ayoub.
“Tukio hili la kuuawa askari ni baya sana. Ni kitendo ambacho
hakikubaliki na mpaka sasa askari zaidi ya 10, wamepoteza maisha, hivyo inatosha,
tutawasaka popote walipo kwa kuwa dawa ya moto ni moto,” alisema.
Alisema tukio hilo la juzi, lilitokea saa 12.15 jioni, maeneo
ya Mkengeni, Kata ya Mjawa, wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, ambapo majambazi,
ambao idadi yao haijafahamika, wakiwa na silaha za moto, walilishambulia kwa
risasi gari la polisi lenye namba PT. 3713, aina ya Toyota Land Cruiser na
kuwaua askari wanane na kumjeruhi mmoja.
Alisema majambazi hao walifanikiwa kuwaua askari hao, baada ya
kuweka mtego na kuanza kushambulia gari walilokuwa wamepanda, eneo hilo ambalo
hakuna makazi ya watu.
Alisema majambazi hao waliwaua askari hao wanane na kumjeruhi
mmoja, huku wakifanikiwa kupora silaha saba, zikiwemo SMG nne na Long Range
tatu.
Kamishna Marijani alisema jeshi hilo sasa linakwenda katika
operesheni maalumu na halitakuwa na mzaha wala msamaha, bali litafanya kile
ambacho kinatakiwa kufanywa.
“Tutawafuata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu,
hakuna atakayepona. Mapambano haya hayana mwisho. askari wetu zaidi ya 10, waliopotea ni wengi
sana, wananchi tunaomba mtuwie radhi, mtuunge mkono katika hili,” alisema.
Aidha, aliwaomba wananchi kutoa taarifa kuliwezesha jeshi hilo
kuchukua hatua stahiki, huku akiwataka wanaofanya ujambazi wa kutumia silaha,
kujua kuwa dawa ya moto ni moto.
JPM
alaani mauaji ya askari
Rais Dk. Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kifo cha
askari hao, huku akiwataka Watanzania wote kutoa ushirikiano ili kukomesha
vitendo vya kuwashambulia polisi, ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya
kulinda raia na mali zao.
"Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari
wetu
wanane, ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa,
"
alisema Rais Magufuli katika salamu zake za rambirambi kwa
IGP Mangu.
Dk. Magufuli alisema anaungana na familia za marehemu wote,
Jeshi
la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha
huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana hao shupavu.
Rais Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa IGP Mangu,
familia za askari wote waliouawa, polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu,” alisema.
Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia polisi, ambao wanafanyakazi
kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na amewataka Watanzania wote watoe ushirikiano katika
kukomesha vitendo hivyo.
CCM
yawalilia polisi waliouawa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa salamu za pole kwa
Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Dk. John Magufuli, kutokana na mauaji ya askari
hao.
Salamu hizo ziliwasilishwa jana, kwa Rais Magufuli na Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akiwa ameambatana na Naibu Katibu Kuu wa CCM Tanzania Bara,
Rodrick Mpogolo na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina
Makilagi, Polepole alisema, kwa kuwa
Mwenyekiti wa CCM ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,
ndio maana CCM imestushwa na tukio hilo na kutoa pole hizo.
Alisema vifo hivyo vinasikitisha, kwa kuwa askari hao wamekuwa na jukumu kubwa
la kulinda usalama wa wananchi na mali zao .
Alisema askari hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira
magumu wakati wote ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama pamoja na mali
zao, hivyo tukio la kuuawa kwao ni jambo la kusikitisha sana.
Aidha, Polepole alisema wamekutana na Rais Magufuli kumueleza
mchakato wa uchaguzi wa ndani wa CCM, ambao unaendelea nchini kote kuanzia
ngazi ya mashina hadi taifa.
Alisema CCM inampongeza Rais Dkt.Magufuli kwa kitendo cha
kizalendo cha serikali ya awamu ya tano,
kutumia fedha zake za ndani katika ujenzi wa reli, itakayokuwa na
kiwango cha kimataifa, yenye urefu wa kilomita 300, kutoka Dar es Salaam hadi
Morogoro.
Alisema ujenzi wa reli hiyo yenye kiwango cha kimataifa,
itakayotumia treni ya umeme, unadhihirisha jinsi CCM inavyojishughulisha na
shida za watu.
Zitto,
ACT nao walaani
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ameelezea hisia zake
kutokana na mauaji ya askari hao kupitia ukurasa wake wa twitter, ambapo
amesema ni muhimu sasa JWTZ waingie kwenye operesheni kwenye eneo hilo.
“Salamu za pole kwa familia za askari wetu. Ni muhimu sasa JWTZ waingie kwenye operesheni maalumu kwenye
eneo hili. Nipo pamoja askari wetu,” alieleza Zitto kupitia ukurasa wake huo.
Wakati
huo huo, Chama cha ACT Wazalendo kimewataka Watanzania kutoa
ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha matendo ya namna
hiyo yanakomeshwa.
Chama hicho kilieleza
hayo kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu, Kamati ya Amani na Usalama,
Mohammed Said Babu, ambaye ilieleza kuwa, chama hicho kimepokea kwa masikitiko
makubwa taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari hao.
“ACT Wazalendo
tunaungana na wito wa kuwataka Watanzania kushikamana na vyombo vya ulinzi na
usalama katika kipindi hiki cha majonzi kwa Taifa na kutoa ushirikiano kwao
kuhakikisha matendo ya namna hii yanakomeshwa.
“Tunachukulia kitendo
hiki kama cha shambulio dhidi ya Jamhuri yetu na hatua kali na madhubuti
zinapaswa kuchukuliwa. ACT Wazalendo tunaamini Jeshi letu la Polisi
litahakikisha linawasaka, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria
wote waliohusika na mauaji haya ya askari wetu,” alisema.
Babu alisema mlolongo
wa matukio ya namna hii unaonyesha kuwa, nchi inapambana na kundi lisilo la
kawaida, hivyo weledi wa hali ya juu unatakiwa katika kukabiliana na tishio
hili.
Pia, alisema Jeshi la
Polisi linatakiwa kufanya kazi zake kwa uangalifu mkubwa na kuepuka kabisa
kuwaingiza raia wasio na hatia kwenye mateso yeyote kwa kuwa adui asipopatikana,
madhara yake ni makubwa zaidi.
“Matukio ya aina hii
katika miezi ya hivi karibuni yawe funzo katika kukabiliana na uhalifu kama
huu. Tunatahadharisha kutotumia mwanya huu kuingiza wasiohusika kwa kuwa
kufanya hivyo ni kuwapa ushindi wahalifu,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment