Sunday, 16 April 2017

BODI, UONGOZI TFC WATUMBULIWASERIKALI imeiondoa madarakani Bodi ya Uongozi na Menejimenti ya Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC Ltd), kwa ubadhirifu wa malipo ya ziada ya sh. bilioni tatu, waliyoyafanya kwa mkandarasi.

Bodi na uongozi wa shirikisho hilo, unatuhumiwa kutafuna shilingi milioni 880, kununua gari aina ya Toyota Prado, kinyume na utaratibu na matumizi ya chama hicho, ambapo viongozi hao walijichukulia mamlaka hayo bila utaratibu.

Uamuzi wa serikali umechukuliwa kwa kuzingatia kifungu cha 126 cha Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013, kutokana na makosa mbalimbali yaliyobainishwa katika uchunguzi uliofanywa juu ya uendeshaji wa shughuli za shirikisho hilo, uliofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika. 
Akizungumza juzi, kwenye mkutano mkuu wa shirikisho la vyama vya ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Tito Haule, alisema kwa mamlaka aliyopewa kisheria, ameiondoa Bodi ya Uongozi pamoja na Menejimenti ya TFC Ltd.

Alisema bodi imeshindwa kuisimamia menejimenti na imekuwa sehemu ya tatizo kwa kubariki au kushiriki vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na viongozi wa shirikisho hilo, ambapo wameamua kuchukua hatua za haraka ili kulinusuru shirikisho hilo.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wana-ushirika kote nchini, kuisoma, kuielewa na kuitekeleza kwa usahihi sheria ya vyama vya ushirika Na. 6 ya Mwaka 2013, ambayo ndiyo inayoainisha uendeshaji wa sekta ya ushirika.

Aidha, Dk. Tizeba amemtaka Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, kutumia mamlaka aliyopewa kisheria, kuhakikisha maslahi ya wana-ushirika yanalindwa na kuwanufaisha wananchi hao, badala ya kuwaachia viongozi wa vyama kujinufaisha wenyewe kutokana na mali zinazopatikana katika vyama hivyo.

Akisoma taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika, Revocatus Nyagilo, alizitaja baadhi ya tuhuma zilizobainishwa katika uchunguzi huo uliofanywa na viongozi hao.

Nyagilo alitaja matatizo hayo kuwa ni pamoja na mchakato wa uuzwaji wa nyumba za shirikisho kutokuwa wazi na bila kuwepo kwa maazimio ya mkutano mkuu, matumizi mabaya ya fedha za mauzo ya nyumba sh. milioni 880, kununua gari (Toyota Prado) kinyume na utaratibu na matumizi mabaya ya fedha za chama sh. bilioni tatu, ikiwa ni malipo ya ziada kwa mkandarasi wa jengo la Ushirika Towers.

Kutokana na kuondolewa madarakani kwa bodi, wajumbe wa mkutano mkuu waliunda bodi ya mpito ili kusimamia uendeshaji wa shirikisho hilo kwa muda.

No comments:

Post a Comment