Tuesday, 17 November 2015

WAOKOLEWA BAADA YA KUKAA ARDHINI SIKU 41





WACHIMBAJI wadogo wa madini watano, waliofukiwa katika mgodi wa Nyangarata, wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wamepatikana wakiwa hai, mmoja akiwa amekufa, baada ya kukaa chini ya ardhi, urefu wa kilometa 100, kwa siku 41.
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, alisema hayo jana, Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa za kupatikana kwa wachimbaji hao.
Alisema juzi mchana, wachimbaji hao walipatikana baada ya kuomba msaada kwa wachimbaji wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao katika shimo lingine, ambapo walipowasikia walitoa taarifa kwa uongozi ndipo wakaokolewa.
Badra  alisema wakati wachimbaji wengine wakiendelea na shughuli zao, walisikia watu wakipaza sauti kwa mbali wakiomba msaada, ndipo walipowauliza kwa wao ni nani na kwamba wakajibu ni wachimbaji waliofukiwa na mchanga mwezi mmoja uliopita.
“Baada ya hapo wale wachimbaji waliweza kuwatambua kuwa ni wale waliofukiwa kipindi cha mwezi mmoja na siku kadhaa, ndipo wakatoa taarifa kwa waliokuwa juu wakaja kuwaokoa,” alisema.
Aliwataja waliookolewa kuwa ni Moses Bulule, Muhangwa Amosi,Chacha Wambura na Msafiri Gerald.
Badra alisema mchimbaji mwingine aliyefahamika kwa jina la Musa Supana, alifariki dunia.
Alisema wachimbaji hao walidai kuwa walipofukiwa, walikuwa wakijitahidi kutoka, lakini tochi ziliishiwa nguvu ya mwanga na kuwalazimu kubaki huko huku wakiishi kwa kula magome ya mizizi ya miti na wakitumia unyevu unyevu wa miamba kama maji.
Alisema wachimbaji hao baada ya kuokolewa, walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama na wanaendelea na matibabu japo hali zao sio mzuri.
Badra alisema wizara inatoa wito kwa wachimbaji wote nchini, kutumia vifaa vya kisasa katika kufanikisha shughuli zao, ambavyo wakati mwingine vitawasaidia kuepuka matatizo kama hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Jibai Mkama, alithibitisha kupokea wachimbaji hao wakiwa hai na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.
Dk. Mkama alisema watu hao waliokolewa jana, saa 12:00 jioni, baada ya wachimbaji waliokuwa wakiendelea na uchimbaji huo kubaini kuwepo kwa watu walikokuwa wakiongea, ndipo walipotoa taarifa kwa viongozi husika.
Alisema majeruhi hao walikuwa wamedhoofika hali zao kutokana na kukosa chakula na hewa safi kwa muda mrefu.
“Tulipata taarifa kutoka katika kituo cha afya  Lunguya, baada ya wao kuarifiwa na wachimbaji hao waliokuwa wakiendelea na shughuli za uchimbaji madini, ndipo walipokwenda kuwachukua na kuwapa huduma ya kwanza kabla ya kuwafikisha hapa hospital ya wilaya,” alisema.
Wachimbaji hao walifukiwa na kifusi cha mchanga Oktoba 5, mwaka huu, na kusababisha vifo vya wachimbaji wengine saba.

No comments:

Post a Comment