Na Joseph Kulangwa
IJUMAA wiki hii, Rais Dk. John Magufuli
anatarajiwa kuzindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kulihutubia kama ilivyo ada kwa miaka yote uzinduzi wa Bunge jipya
unapofanyika.
Ni wakati ambao Rais atatumia fursa
hiyo adhimu kulitangazia Taifa nini anakusudia kulifanyia katika kipindi chake
cha miaka mitano ya urais, baada ya Watanzania walio wengi kumpa ridhaa ya
kuwaongoza.
Macho na masikio ya Watanzania
yataelekezwa Dodoma, ambako ndiko uzinduzi huo unafanyika, ambapo pia wabunge
wapya na wa zamani watapata fursa ya kukutana na kufahamiana zaidi.
Kama ilivyo miaka yote, Bunge la safari
hii pia litakuwa na idadi kubwa ya wabunge wa CCM, ambao kwa vyovyote watakuwa
na mtihani wa kupambana kwa hoja na wenzao wa vyama vya upinzani vya CUF,
Chadema, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo.
Wakati maandalizi ya kikao hicho cha uzinduzi
yakiendelea, mchakato wa kumpata Spika na Naibu Spika nao unaendelea ili siku
ya siku ikifika viongozi hao wa Bunge wawe wamechaguliwa.
Tayari CCM imeshampitisha mbunge wa
Kongwa, Job Ndugai kuwa mgombea wake wa nafasi ya Uspika. Katika bunge lililopita,
Ndugai alikuwa Naibu Spika.
Kamati ya wabunge wa CCM iliamua
kumpitisha Ndugai kuwa mgombea wa nafasi hiyo, baada ya wagombea wengine
wawili, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulla Mwinyi na Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson kuamua kujitoa.
Taratibu hizo zinafanywa huku tayari
aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya
Chadema, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward
Lowassa ametoa tamko lake kuhusu uchaguzi mkuu.
Akizungumza na wanahabari juzi, Lowassa
alisema matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yakimpa
ushindi aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli si
halali. Lowassa akasema alichopoteza ni pambano, lakini hajashindwa vita.
Tofauti na alivyopata kusema huko nyuma
baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba
akishindwa atarejea kijijini Monduli kuchunga mifugo yake, safari hii amesema
atajikita zaidi katika kuendeleza mapambano ya kisiasa.
Alisema chini ya Katiba ya sasa ya
nchi, ni dhahiri uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki na hivyo atapambana ili
kupatikana Katiba mpya, ambayo itatoa mwongozo mzuri utakaowezesha kuundwa kwa
tume huru ya uchaguzi.
Ikumbukwe kuwa yeye ni miongoni mwa
waliokataa Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba, lakini sasa baada ya
kushindwa urais, anaiona ni njema na anaitetea ili iandikwe kwa mwelekeo ambao
awali aliukataa.
Katika msimamo wake mwingine kutokana
na kutotambua matokeo yaliyotangazwa na NEC na kwa kuwa Katiba hairuhusu
matokeo hayo kupingwa mahakamani, yeye na Ukawa hawautambui urais wa Dk
Magufuli.
Msimamo wa Lowassa unashajiishwa na wa
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye amekaririwa akisema watapinga
hata hotuba ya Dk Magufuli ya uzinduzi wa Bunge la 11 na safari hii si kwa
kutoka nje, bali kwa kusimama wakati wote akihutubia ili kupinga yaliyomo
katika hotuba hiyo na nafasi yake ya urais.
Katika hotuba zake zote za kampeni na
hata ya kutoa shukurani siku anaapishwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam,
Novemba 5, mwaka huu, Rais Magufuli alisema hatabagua Watanzania kwa itikadi
zao na kuwataka wanasiasa kukubali matokeo na kuungana naye kuwasaidia
wananchi.
Mara zote Rais Magufuli alisisitiza
kuwa yeye ni Rais wa wote na si wa CCM tu kwa kuamini kwamba, jukumu alilonalo
ni la kuwasaidia Watanzania bila kujali waliompigia au waliomnyima kura, kwa
kuwa wote wana haki ya kuishi katika nchi hii na kuhudumiwa kwa usawa.
Kwa kuwa Rais aliwasihi Watanzania kuwa
wamoja na kuacha kubaguana, lingekuwa jambo jema kama wangemwelewa na kukubali
hisia zake za moyoni na kumpa miaka yake mitano athibitishe kauli zake na si
kumwekea vikwazo ambavyo vitamnyong’onyeza.
Wapinzani hususan wa Ukawa, wanapaswa
kuelewa kuwa mwisho wa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi mwingine, na kwamba miaka
mitano si mingi, hivyo kusubiri hadi 2020 si tatizo na wavute subira wakati huo
ukifika waingie ulingoni kujaribu bahati nyingine.
Kitendo cha kuingia bungeni na kusimama
wakati wote ambao Rais atakuwa anahutubia, kwanza ni kinyume na kanuni za Bunge,
lakini pia ni kumkosea adabu mtu ambaye amechaguliwa na Watanzania asilimia 54
ya waliopiga kura.
Kumfanyia dhihaka na dharau Rais ni
sawa na kuwafanyia dhihaka na dharau Watanzania wote waliomchagua, ni vema basi
wakamsikiliza Rais na kumpa fursa ya kuzindua Bunge kwa utulivu na hasa
ikizingatiwa kuwa wabunge wa Ukawa nao watakuwa ndani.
Mimi sidhani kuwa kusimama bungeni kuonyesha
kumpinga Rais na serikali yake ni jambo lenye siha kwa mustakabali wa Taifa,
bali ni kutaka kuonyesha jeuri ambayo haitazaa matunda yoyote.
Mwaka 2010, aliyekuwa mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema, Dk Wilbrod Slaa, alikuja na msimamo kama huo. Baadhi ya
wabunge wa upinzani nao kwa pamoja wakaamua kutoka nje na kuwaacha wa CCM, UDP
na TLP, wakimsikiliza Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge hadi mwisho.
Hata hivyo, waliotoka nje walirejea
siku nyingine na kuendelea na Bunge kama kawaida na hatimaye Rais Kikwete
aliendelea kuongoza Taifa kwa miaka mingine mitano ya awamu ya pili na kumaliza
salama Novemba 5, mwaka huu.
Kwa kurejea hilo, ni matumaini ya
Watanzania wengi kuwa wapinzani safari hii wataiona mantiki na kukubali
kumsikiliza Rais Magufuli wakiwa wamekaa na kutafakari ujumbe atakapokuwa
anawasilisha, badala ya kukaidi kanuni za Bunge eti kwa sababu hawatambui
ushindi wake.
Watanzania wasio wabunge wana hamu ya
kumsikiliza Rais wao mpya na kujua anawaahidi kitu gani katika kukabiliana na
matatizo na kero walizonazo. Bila shaka hawana haja ya kushuhudia malumbano
kati yake na wabunge wasioamini wala kukubali ushindi wake.
Ni bora hata wakaacha kuingia bungeni
ili walio tayari kumsikiliza wamsikilize, lakini kama watang’ang’ania
walichopanga kufanya, basi bila shaka Katibu wa Bunge na uongozi mzima wa Bunge
wataona nini cha kufanya ikiwa ni pamoja na kuangalia suala la posho zao.
No comments:
Post a Comment