Monday 22 August 2016

WANA-CCM WAASWA KUTOOGOPA KUWAKOSOA VIONGOZI WABOVU



WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, wameaswa kuacha tabia ya kuogopa kuwakosoa au kuwaeleza ukweli viongozi wao pale wanapokwenda au kutenda kinyume na katiba, kanuni na taratibu za Chama.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Erasto Kwilasa, alipokuwa akizungumza katika kikao cha ndani cha viongozi wa CCM wa kata na wilaya.

Kwilasa alikuwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 katika wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Alisema tabia ya wanachama wa CCM kuogopa kuwaeleza ukweli viongozi wanaokwenda kinyume na maelekezo ya katiba au kanuni za Chama, imechangia manung’uniko ya chini chini yanayosababisha mgawanyiko miongoni mwao na kuendeleza tabia ya kupigana majungu.

Alisema CCM sio mali ya viongozi bali ni ya kila mwanachama na mwanachama yeyote anayo haki sawa na wanachama wengine kwa mujibu wa katiba, hivyo mwanachama anayo haki ya kutoa maoni, kushauri na kukosoa pale atakapoona mambo hayaendi sawa au kuwepo kwa kiongozi anayekwenda kinyume cha utaratibu.

“Chama cha Mapinduzi sio mali ya viongozi au kiongozi yeyote, ni mali ya wana CCM wote, hivyo hakuna sababu ya kiongozi kuogopwa kuelezwa ukweli inapobainika anakwenda kinyume au anavunja katiba na kanuni tulizojiwekea, tukiwaogopa na kuzungumza pembeni, hayo ndiyo tunayoyaita majungu.

“Hakuna sababu ya wana CCM kuogopana, chama hiki bado ni chama imara sana, hakitayumba wala kuyumbishwa na yeyote, labda wanachama wenyewe turuhusu mipasuko miongoni mwetu na hii inaweza kutokea iwapo tutaendeleza makundi. Ndugu zangu makundi ndani ya chama ni hatari kwa uhai wa chama chetu,” alieleza.

Aliongeza kuwa baada ya Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa rasmi mikoba ya uenyekiti wa CCM Taifa, ameahidi kufanya kila linalowezekana kuona Chama kinaimarika zaidi kwa kusafisha mapungufu yote yaliyokuwepo huko nyuma ili kurejesha imani ya Watanzania kwa CCM.

“Rais wetu na mwenyekiti mpya wa taifa, Dk. Magufuli ameeleza wazi dhamira yake ya kukijenga chama chetu ili kiwe imara zaidi na ametuahidi kutotuangusha wana-CCM, anataka CCM iwe ni ile inayowajali wanyonge na hatakuwa tayari kuona wananyanyaswa, hivyo na sisi tumuunge mkono, tutumie vikao katika kujadili mambo yetu,” alieleza Kwilasa.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo wa mkoa, aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na Khamis Mgeja, alitoa wito kwa wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi utakaofanyika mwakani, kuanzia ngazi ya mashina hadi taifa.

Kwilasa alisema uchaguzi ujao ndani ya CCM, utakuwa huru na wa wazi kwa kila mwana CCM, aliyetimiza sifa za uongozi na hapatakuwepo, masuala ya rushwa, hivyo hakuna sababu za wanachama wasio na uwezo wa kifedha kuogopa kuchukua fomu za kuomba kugombea kwa kuwaogopa watu wenye fedha.

“Sote tumemsikia mwenyekiti wetu alipokuwa akikabidhiwa mikoba rasmi ya kukiongoza chama chetu, moja ya mambo aliyoyakemea kwa nguvu zake zote ni rushwa. Alisema wazi katika uchaguzi ujao, mwanachama yeyote atakayebainika kuomba uongozi kwa kutoa rushwa, jina lake litakatwa bila kujali uwezo wake wa kifedha.

“Ukweli ndugu zangu mambo ya kupokea fedha za wagombea yalichangia sana mgawanyiko miongoni mwetu, maana mtu anamwaga fedha zake halafu anakosa uongozi, hii ilichangia watu waliokuwa kwenye kambi yake wajenge chuki na kambi iliyoshinda, hivyo safari hii hakuna rushwa, jitokezeni kugombea,” alieleza Kwilasa.

No comments:

Post a Comment