Monday 22 August 2016

NDIKILO AWASIMAMISHA KAZI MAOFISA MKURANGA

MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, amewasimamisha kazi maofisa ardhi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa matumizi mabaya ya ofisi.

Mwenyekiti huyo amemsimamisha kazi Ofisa Ardhi Mteule wa halmashauri hiyo, Riziki Chagie na Ofisa Ardhi, Mussa Kichumu ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola.

Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watumishi hao na kuwaweka ndani ili hatua zingine ziweze kuchukuliwa.

Mhandisi Ndikilo, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, aliyasema hayo wakati kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapa, ilipokwenda kufuatilia utaratibu uliotumika kumegwa hekari 30, katika shamba namba 1,691, lililoko Mwandege  na kupewa Kampuni ya Bakhresa Food Products kwa gharama ya sh. milioni 458.

Mhandisi Ndikilo alimuagiza Katibu Tawala (RAS) wa mkoa wa Pwani, Zuberi Samataba, kutenga fedha za kuwahamisha watumishi wengine wa idara ya ardhi ndani ya halmashauri hiyo kwa kuwa wanadaiwa kuigeuza ofisi hiyo kuwa kitega uchumi kwa maslahi yao binafsi.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo iliketi na kupitia nyaraka zote, baada ya kumuagiza mkuu wa wilaya kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya wilaya hiyo inayohusu umiliki wa shamba hilo.

Mbali na mkuu wa wilaya, alisema ofisi yake pia ilihitaji taarifa za mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo na ofisa ardhi mteule, ambapo baada ya majadiliano ndani ya kamati hiyo, walikubaliana kutembelea eneo husika na kukaa na pande zote.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoa, ililazimika kwenda kufuatilia taarifa iliyoipata kuhusu kumegwa kwa ekari 30, za shamba la Youth with A Mission na kugawiwa kwa kampuni ya Bakhresa Food Products, ambayo ililipa sh. milioni 458, jambo lililozua utata.

Kamati hiyo ilishangazwa na kampuni hiyo kutoa fedha hizo wakati thamani ya ekari 30 kwa sasa ni sh. bilioni 4.749, ambazo zingeweza kutumika katika matumizi mbalimbali ya jamii, ikiwemo kujenga madarasa, stendi, shule na kununulia madawati.

Mhandisi Ndikilo alisema mchakato mzima wa uuzaji ardhi hiyo hauna maslahi mapana kwa halmashauri wala wilaya, bali ulilenga kutunisha mifuko ya baadhi ya watumishi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kuwa karibu katika kufuatilia masuala nyeti kama hilo, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwa serikali.

No comments:

Post a Comment