Monday 22 August 2016

SERIKALI KUPIMA ARDHI, KUMILIKISHA WANANCHI


SERIKALI imesema imejipanga kuwawezesha wanachi wanyonge kiuchumi kupitia upimaji ardhi zao nchi nzima na kumilikishwa kihalali ndani ya miaka 10.

Imesema hatua hiyo inalenga kutambua thamani ya raslimali hiyo, ikiwa ni mojawapo ya njia za kukabiliana na migogoro ya ardhi hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipotembelea ofisi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Kagera, kisha kutembelea mradi wa ujenzi wa nyumba 20, zitakazouzwa kwa gharama nafuu wilayani Chato, Geita.

“Mkuu wa Mkoa wa Kagera nakushauri kwa mwaka huu wa fedha, hakikisheni mnawapimia wananchi na kutoa hati elfu 10, kwa mkoa mzima. Hii inawezakana kabisa. Pia wilaya ya Chato, nakuagiza mkuu wa wilaya pimeni na pangeni mji. Mwaka huu wa fedha toeni hati 5,000. Hiyo itasaidia kuongeza mapato na kuweka miji katika mandhari nzuri ili kuvutia wawekezaji na kuondokana na migogoro ya ardhi.

“Tunafanya hivyo ili kila eneo lijulikane lipo kwa madhumuni gani, jambo ambalo litaondoa migogoro ya kila siku, hususan kwa wakulima na wafugaji, ambayo wakati mwingine imekuwa ikisababisha vifo na uvunjifu wa amani katika jamii,"alisema.

Alisema bila kupima ardhi, kumilikisha na kuwapatia wananchi hati miliki zilizo salama, hadithi ya kuwanyooshea wananchi vidole na kusema wamejenga kiholela itaendelea.

Waziri Lukuvi aliagiza ndani ya mwezi mmoja, maeneo yote ya serikali yawe yamepimwa na kupewa hatimiliki, yakiwemo ya taasisi kama vile shule, hospitali na majeshi, kwani kwa sasa imegundulika wapo baadhi ya watu wameanza kujipenyeza na kujenga ndani ya maeneo hayo.

Mbali na hilo, Lukuvi aliipongeza NHC mkoa wa Kagera kwa kupandisha mapato kwa mwaka huu wa fedha, kutoka sh. milioni 73 hadi sh. milioni 83, kwa kipindi kifupi na kuwataka kutopandisha kodi kwa wapangaji wake bali waongeze miradi itakayopandisha mapato yao.

No comments:

Post a Comment