Monday, 22 August 2016
KACHERO WA POLISI AUAWA KIKATILI MWANZA
KACHERO wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoani Mwanza, PC John Nyange, mwenye namba G. 5092, ameuwa kwa kuchomwa kisu shingoni katika eneo la klabu ya Villa Park Resort, jijini Mwanza.
Habari zilizopatikana hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi, zimesema tukio la mauaji ya askari huyo lilifanyika saa 10:00 usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo inadaiwa kuwa lilifanyika wakati mamia ya watu wakiselebuka katika tamasha la Fiesta, lililoandaliwa na Kampuni ya simu za mikononi ya TIGO, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jirani na klabu hiyo.
Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo (hakutaka jina liandikwe gazetini), alidai kabla ya kwenda Villa Park, kachero huyo aliyekuwa kwenye pilika pilika za tamasha la Fiesta, lililoanza saa 12:00 alfajiri jana, alichomwa na kisu shingoni na kumsababishia kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha alilopata.
Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, PC Nyange alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Stephano Memorial Universty cha mjini Moshi, akisomea Shahada ya Sayansi ya Habari na Mawasiliano.
Alisema kwa muda mrefu marehemu alikuwa na ugomvi na fundi wa kompyuta yake (laptop), aliyemtaja kwa majina ya Hussein Seleman Maginga (27), ambapo jana, walikutana na mtuhumiwa akiwa na wenzake watano eneo la Villa Park Resort.
“Ndipo walipomvamia, wakamchoma shingoni kwa kitu chenye ncha kali, alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa ajili ya matibabu ya jeraha hilo, lakini bahati mbaya akafariki akiwa njiani,” alieleza kamanda huyo.
Msangi aliongeza kuwa marehemu alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Stephano Memorial, akisomea Teknolojia ya Mawasiliano (IT) na kwamba, mauti yamekuta akiwa ameruhusiwa kwenda kusalimia familia yake iliyoko Mwanza.
Alisema kuwa mtuhumiwa wa mauaji haypo, Magina, mkazi wa Kigoto Kirumba, katika Manispaa ya Ilemela, anashikiliwa pamoja na wenzake watano.
Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, jeshi la polisi lilikuwa likiendelea kuwahoji ili kupata ukweli wa tukio hilo na kwamba, ushahidi ukipatikana, watafikishwa mahakamani.
Kamanda Msangi alisema jeshi hilo limesikitishwa na kifo hicho cha askari huyo, ambaye alikuwa bado kijana, akitegemewa zaidi kutumikia taifa na familia yake.
Amewaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kosa la jinai, vinginevyo watakabiliwa na mkondo wa sheria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment